" SHERIA ZIPO, USALAMA KITENDAWILI MIGODINI

SHERIA ZIPO, USALAMA KITENDAWILI MIGODINI


Na Mapuli Kitina Misalaba, Shinyanga

 

Licha ya kuwepo kwa sheria, kanuni na mifumo ya usimamizi wa sekta ya madini nchini, simulizi kutoka migodi ya wachimbaji wadogo mkoani Shinyanga zinaonyesha taswira tofauti—usalama bado ni kitendawili kisichopata majibu.

 

Katikati ya hali hiyo, sauti ya mtaalamu wa jiolojia, James Kibiti Muiko, inajitokeza ikiweka wazi kuwa tatizo si ukosefu wa sheria bali utekelezaji wake. Kibiti kwa mtazamo wake, changamoto si ukosefu wa sheria bali ni pengo kati ya sheria na utekelezaji wake. Ni pengo linalogharimu maisha.

 

“Hatua za awali za utoaji leseni hufuata taratibu zote, lakini matatizo huanza mara uchimbaji unapoanza na usimamizi kuwa dhaifu,” anasema Kibiti ambaye ni Mjiolojia kutoka Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi, Shinyanga

 

Ripoti ya Tume ya Madini nchini (TMC) ya mwaka 2023/24  inaonyesha kuwa kutokufuatwa sheria za madini ni changamoto kubwa kiasi cha kuilazimisha tume hiyo kutoa notisi za ukiukwaji na hata kufuta leseni za wahusika mara kwa mara.

 

Sheria zinazotazamwa kusimamia usalama wa wachimbaji wadogo ni ile ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 (OSHA) na Sheria ya Madini ya mwaka 2010, lakini bado kuna udhaifu katika kusimamia na kulinda usalama wa wachimbaji hao.

 

Ingawa sheria hizi zimekusudiwa kuweka misingi ya usalama kazini na katika shughuli za uchimbaji, uhalisia unaonyesha kuwa hazijitoshelezi kukidhi mazingira halisi ya uchimbaji mdogo (ASM), ambao kwa kiasi kikubwa ni sekta isiyo rasmi, yenye rasilimali chache, na inayofanyika nje ya mifumo madhubuti ya kisheria.

 

Kwa ujumla, udhaifu wa sheria hizi mbili unatokana na kutolingana na hali halisi ya uchimbaji mdogo, ukosefu wa masharti mahsusi ya usalama, utegemezi wa kanuni zisizo wazi, pamoja na changamoto za utekelezaji. 

 

Matokeo yake wachimbaji wadogo nchini Tanzania wanaendelea kufanya kazi katika mazingira hatarishi, wakikosa ulinzi madhubuti wa kisheria licha ya uwepo wa sheria hizo.

 

Mwenendo wa ajali

Takwimu zinaonysha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2022 hadi 2025, watu 72 waliathirika na ajali migodini katika maeneo ya Nyandolwa na Mwakitolyo; kati yao 36 walifariki dunia. Ajali ya Agosti 11, 2025 pekee iligharimu maisha ya watu 21 kati ya 25 waliohusika—siku ambayo kwa wengi ilibadili “miduara” kuwa makaburi ya wazi.

 

Kwa mujibu wa Kibiti, moja ya vyanzo vikuu vya ajali ni “miduara”—mashimo ya uchimbaji chini ya ardhi. “Mara nyingi huchimbwa pasipo utaalam, hali inayosababisha mtikisiko na maporomoko ya ghafla,” anaeleza. Tofauti na migodi mikubwa, wachimbaji wadogo huchimba kwa ukaribu mkubwa, jambo linaloongeza hatari ya miundombinu kuingiliana chini kwa chini bila udhibiti.

 

Hatari hii huongezeka zaidi kutokana na uwepo wa kundi linalojulikana kama “manyani”—watu wanaoingia kwenye miduara iliyofungwa kwa ukarabati wakisaka mabaki ya madini. Ni taswira ya kukata tamaa; uchumi wa kuungaunga unaowasukuma watu kwenye hatari iliyo wazi.

 

Hata hivyo ripoti ya TMC ya 2023/24 inabainisha kutokuwepo kwa takwimu za kina kuhusu ajali, huku kukiwa hakuna idadi rasmi ya vifo, majeruhi, wala aina za ajali. Kwa wataalamu, hili ni pengo linalodhoofisha uwezo wa kupanga sera za usalama.

 

Hali hiyo inathibitshwa na baadhi ya viongozi wa vijiji ambao wanakiri kuwepo kwa utamaduni wa kufumbia macho ajali. Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandolwa, Mange Didas, anasema, “Vifo vya mtu mmoja au wawili mara nyingi haviripotiwi.” Hali hii inaficha ukubwa wa tatizo na kuchelewesha hatua.

 

Sababu za ajali

Taarifa ya Tume ya Madini nchini (TMC) kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2024 unabainisha kuwa miongoni mwa visababishi vya ajali katika migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ni kuporomoka kwa migodi, ukosefu wa miundombinu salama ya uchimbaji, matumizi ya zana duni au za kienyeji, pamoja na kukosekana kwa mifumo ya uingizaji hewa.

 

“Teknolojia nayo ni changamoto. Wachimbaji wengi bado wanatumia mbinu za jadi na vifaa visivyo salama—hali inayoongeza uwezekano wa ajali,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya mwaka unaoishia Juni 30, 2024.

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika migodi mingi ya wachimbaji wadogo hakuna vifaa kinga (kama chepeo/helmeti na buti), wala mfumo thabiti wa ukaguzi wa mara kwa mara. Hali hii inaacha wachimbaji wakifanya kazi katika mazingira yasiyo na ulinzi.

 

Hali hii inathibitishwa na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini katika migodi ya Nyandolwa na Mwakitolyo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambao mbali na kutokuwa na vifaa vya usalama, pia wamekuwa wakiingia migodini bila kupata mafunzo stahiki.

 

Miongoni mwao ni Boniface Misong’oni ambaye anasema vifaa vya kujikinga vinapotolewa, hakuna mwongozo wa matumizi yake. “Unapewa vifaa, lakini hakuna anayekuonyesha jinsi ya kuvitumia ipasavyo,” anasema.

 

Hata hivyo Clement Samson anasema baadhi ya wachimbaji huwa hawazingatii a matumizi ya vifaa vya kujikinga, hali inayoongeza hatari.

 

Naye Mpiga Mhamal anaeleza kuwa wanapokuja wachimbaji wapya mara nyingi huulizwa iwapo ana uzoefu na akijibu ndiyo, huruhusiwa kuanza kazi mara moja. “Ukosefu wa mafunzo ya awali unasababisha wachimbaji kufanya kazi kwa tahadhari ndogo,” anasisitiza.

 

Kwa upande wa wanawake, hali si tofauti. Christina Shija na Stella Jemes wanaojihusisha na ubondaji wa mawe ya dhahabu, wanasema wanategemea mbinu za jadi kujilinda. “Hatupati mafunzo rasmi ya usalama,” wanasisitiza, wakieleza kuwa ajali ndogondogo huathiri afya zao na kipato cha familia.

 

Mwingine ni Kulwa Mpelwa ambaye  anasema: “Naingia ndani ya duara nikitegemea nilichojifunza kwa wenzangu.” Kauli hii inaonyesha pengo kubwa la mafunzo rasmi ya usalama kwa wachimbaji.

 

Kandya Ndutu yeye anaongeza kwa kusema, “Elimu ya usalama haipatikani, tunajifunza kwa majaribio na makosa.”

 

Udhaifu wa Sheria ya OSHA

Sheria ya OSHA ya mwaka 2003 inazungumzia mazingira rasmi ya kazi yenye muundo wa mwajiri na mwajiriwa. Hali hii haipo katika uchimbaji mdogo ambapo wachimbaji wengi hujiajiri au kufanya kazi katika vikundi visivyo rasmi.

 

Kutokana na hilo, vifungu muhimu vya sheria vinavyohusu wajibu wa mwajiri, usimamizi wa usalama, na uwajibikaji vinashindwa kutekelezwa kwa vitendo. Pia sheria inalazimisha usajili rasmi na ukaguzi wa mara kwa mara, jambo ambalo wachimbaji wadogo wengi hawawezi kulimudu kutokana na gharama na urasimu, hali inayowasukuma kufanya kazi nje ya mfumo wa kisheria.

 

Kadhalika matakwa yanayowekwa na sheria hiyo kama matumizi ya mitambo iliyothibitishwa, uwepo wa wataalamu wa afya kazini, na ukaguzi maalum ni kama mfupa mgumu kutafunwa kwa kundi hili la wachimbaji wadogo, hivyo kuifanya sheria ionekane kuwa ya kinadharia zaidi kuliko ya vitendo, hasa katika muktadha wa ASM.

 

Hata pale ambapo sheria inatoa masharti muhimu ya usalama kama vile matumizi ya vifaa kinga, huduma ya kwanza, na udhibiti wa hatari, utekelezaji wake unakuwa hafifu kutokana na ukosefu wa ufuatiliaji na hofu ya wachimbaji kuripoti ajali kwa kuhofia adhabu.

 

Ukaguzi wa usalama

Uchunguzi wa Misalaba Media pia ulibaini udhaifu wa ukaguzi wa usalama katika migodi, kabla ya kutumia.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyandolwa, Mange Didas, anasema, ukaguzi wa mara kwa mara haupo. “Wakaguzi wanapaswa kufanya kazi mara kwa mara, lakini wengi hawalipwi au hawafanyi kazi ipasavyo.”

 

Naye Nuhi Shomi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwakitolyo, anaeleza kuwa maofisa wa madini hufika mara chache na wakati mwingine hawashuki kabisa kwenye miduara. “Usimamizi unakuwa wa juu juu,” anasema.

 

Hata hivyo wakaguzi wa migodi nao wanajitetea, wakisema nao hawawezeshwi kufanya kazi zao ipasavyo nakwamba mafunzo wanayopata hayatoshi.

 

“Tunapatiwa mafunzo mara moja kwa mwaka, hayatoshelezi,” anasema mmoja wa wakaguzi Samson Jelemiah huku mwezake Dotto Seleman akiongeza kuwa hata taarifa wanazotoa huwa hazifanyiwi kazi kwa wakati.

 

Hata hivyo Sheria ya Madini ya mwaka 2010, licha ya leseni za uchimbaji mdogo (PML), haijaweka masharti ya moja kwa moja yanayolenga usalama wa wachimbaji hao. Badala yake, inatoa marejeo ya jumla tu kwa kanuni nyingine zisizobainishwa wazi, hali inayosababisha ukosefu wa mwongozo thabiti wa usalama.

 

Aidha, sheria haielezi wazi wajibu wa wachimbaji au mamlaka husika katika kuhakikisha mazingira salama ya kazi, wala haiweki masharti ya lazima kuhusu mafunzo ya usalama, matumizi ya vifaa kinga, au utaratibu wa kuripoti ajali. Upungufu huo unaacha pengo la kisheria linalowaacha wachimbaji wadogo katika hatari bila ulinzi wa kutosha.

 

Hata nafasi ya Mkaguzi Mkuu wa Migodi, ingawa ipo kisheria, haijapewa mamlaka ya moja kwa moja ya kusimamia na kutekeleza masuala ya usalama kwa wachimbaji wadogo, hivyo kuwapo umuhimu wa sheria hiyo kurejewa.

 

Mwisho


 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post