
Na Mapuli Kitina Misalaba, Shinyanga
Sauti za vilio, hofu na taharuki zimekuwa sehemu ya simulizi za wachimbaji wadogo katika maeneo ya Nyandolwa na Mwakitolyo, mkoani Shinyanga. Ni maeneo ambayo chini ya ardhi yake kuna matumaini ya dhahabu, lakini juu yake kuna wingu la vifo vinavyojirudia mara kwa mara.
Katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2022 hadi 2025, takwimu zinaonyesha kuwa watu 72 wameathirika na ajali migodini katika maeneo haya mawili. Kati yao, 36 wamefariki dunia, mmoja hajapatikana, 11 wamejeruhiwa na 27 wamenusurika.
Ajali ya Agosti 11, 2025 katika mgodi wa Nyandolwa ndiyo iliyobeba uzito mkubwa zaidi wa majonzi. Watu 25 walihusika, ambapo 21 walipoteza maisha papo hapo katika tukio lililoacha alama isiyofutika kwa wakazi wa eneo hilo. Kwa wengi, siku hiyo iligeuza “miduara” kuwa makaburi ya wazi.
Miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Samwel Makenzi Chembanya (26) ambaye aliacha vilio kwa familia yake; mke na watoto wawili pamoja na mama yake mzazi, aitwaye Angess Makenzi ambaye anasema mtoto wake alikuwa akifanya kazi ya uchimbaji mgodini kama ajira rasmi, akijihusisha pia na kazi za kufunga magogo ndani ya maduara.
Maduara ni mashimo makubwa yanayochimbwa kufikia dhahabu chini ya ardhi, hivyo Samweli alikuwa mmoja wa wataalamu wa kufunga nguzo ambazo huwekwa ili kuzuia hatari ya kuporomoka kwa ardhi na kusababisha maafa vikiwamo vifo.
Bibi Agness anasema siku ya tukio, ilikuwa Jumatatu saa nne asubuhi, walipokea taarifa kuwa maduara yameporomoka na kwamba huenda Samwel alikuwa miongoni mwa waliokuwa ndani. Mama huyo anasema walifika eneo la tukio na kushuhudia hali halisi, huku juhudi za uokoaji zikiendelea kwa siku kadhaa bila mafanikio ya haraka.
“Ilichukua zaidi ya siku kumi ndipo mwili wake ulipopatikana akiwa tayari amefariki dunia,” anasema Agness kwa huzuni. Anaongeza kuwa walilazimika kuuchukua mwili huo kwa ajili ya mazishi, huku ukiwa umeharibika vibaya, na kwamba katika kipindi chote hicho hawakupata msaada wa kutosha wala kumuona mwajiri wa marehemu akishiriki katika msiba.
Kwa mujibu wa familia hiyo, siku chache baada ya mazishi, mke wake alilazimika kuondoka na kurejea makwao akiwa na watoto, hali iliyoongeza mzigo wa malezi na maisha kwa familia zote mbili. Familia ya marehemu Samwel inasema kifo hicho kimewaacha katika hali ngumu ya kiuchumi kwani walikuwa wakimtegemea marehemu kwa mambo mengi.
Kuna hatua za mabadiliko?
Kila ajali mpya si tu inapoteza maisha ya wachimbaji, bali pia huacha maswali kuhusu usalama, uwajibikaji na nafasi ya mamlaka za serikali katika kulinda maisha ya Watanzania wanaotegemea sekta hii kujikimu.
Kwa upande mwingine, miduara chini ya ardhii, imekuwa kiini cha ajali kwani mara nyingi huchimbwa bila utaalamu wa kutosha, huku umbali kati ya duara moja na jingine ukipunguzwa ili kuongeza uzalishaji. Matokeo yake ni maporomoko ya ghafla yanayofukia wachimbaji hai.
Akiwa ziarani mkoani Geita Februari mwaka 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Uhusiano), Deus Sangu alisema: “Tumekuwa tukipata taarifa za matukio mengi ya ajali hususan kwa wachimbaji wadogo kufukiwa na vifusi wakiwa wanatekeleza majukumu yao”.
Sangu alikuwa akizindua mafunzo kwa wajasiriamali wadogo wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (WAWABU) wanaofanya shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Bukombe.
Mafunzo hayo ni sehemu ya programu za uhamasishaji masuala ya usalama na afya kazini kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Aprili 28, 2026.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Shinyanga, Mhandisi Noel Baraka, anasema baada ya ajali ya Agosti 11, 2025 katika mgodi wa Nyandolwa Serikali ilizisimamisha kwa muda leseni mbili katika eneo hilo ambazo ni za kikundi cha Wachapakazi na ile ya HHH and Partners.
Baraka anasema kabla ya ajali, leseni ya Wachapakazi ilikuwana maduara 66 yaliyokaguliwa; 44 yakibainika kuwa hatarishi na hivyo kufungwa, huku 22 yakiruhusiwa kuendelea na uzalishaji baada ya kukidhi vigezo vya usalama.
“Kwa upande wa HHH and Partners, kampuni hiyo ilikuwa na maduara 26; kati yake 19 yalionekana kuhatarisha usalama wa wachimbaji na kufungwa, na saba pekee ndiyo yameruhusiwa kuendelea na uzalishaji mara moja baada ya kutekeleza maelekezo ya wataalamu,” anasema Baraka.
Kwa leseni ya HHH and Partners, alisema wameruhusu maduara saba tu kuendelea na shughuli na hawaruhusiwi kuongeza duara jingine lolote na kwamba mkaguzi wa Tume ya Madini amewekwa eneo hilo kusimamia kazi zinazofanyika kila siku ili kuzuia uzembe wa awali wa kuongeza maduara kiholela.
Anasema kwa mujibu wa kanuni za usalama, umbali kati ya duara na duara haupaswi kupungua mita kumi na kwamba Ofisi ya Madini inaendelea kusimamia Kanuni za Usalama na Utunzaji wa Mazingira Mahali pa Kazi za mwaka 2010, ambazo zinataka umbali huo uzingatiwe.
Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 imempa mamlaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), kusimamia usalama kazini, kufanya ukaguzi na kuhakikisha mazingira ya kazi ni salama.
Jitihada za kuwapata OSHA kuzungumzia hali ya usalama katika migodi na kujibu lawama za kushindwa kusimamia na kutoa elimu kwa wachimbaji zimekwama kwa zaidi ya miezi miwili kwani kila walipofikiwa kupitia kwa ofisa habari wake, Paul Gyuna alihahidi kutoa majawabu, ahadi ambayo hata hivyo hakuwahi kuitekeleza.
Hata hivyo Mwezi Februari akizungumza kwenye mafunzo ya Wawabu, Bukombe mkoani Geita, Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda alisema OSHA imekuwa ikitekeleza programu ya mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo ili kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya na kuongeza kiwango cha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya nchini.
Mbali na OSHA, Ofisi za Madini katika ngazi za mikoa pia zina jukumu la kuratibu shughuli zote za uchimbaji na kuhakikisha masharti ya leseni yanafuatwa, ikiwa ni pamoja na masuala ya afya na usalama migodini.
Hata hivyo kwa mujibu wa wataalamu wa sekta ya madini, changamoto kubwa haiko kwenye uwepo wa sheria, bali utekelezaji wake.
James Kibiti Muiko, Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Shinyanga, anaeleza kuwa hatua za awali za kutoa leseni hufuata taratibu zote, lakini matatizo huanza pale uchimbaji unapoanza na usimamizi kuwa dhaifu.
MWISHO…………………………….
Afisa
Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Shinyanga, Mhandisi Noel Baraka, akizungumza na Misalaba Media ofisini kwake. SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment