" UCHAMBUZI: AMANI, SHERIA NA UKWELI WA MATUKIO YA OKTOBA 29, 2025

UCHAMBUZI: AMANI, SHERIA NA UKWELI WA MATUKIO YA OKTOBA 29, 2025

Amani ni msingi wa ustawi wa taifa lolote. Bila amani, haki nyingine zote za msingi hupoteza maana yake. Hii ndiyo taswira inayojitokeza wazi kupitia ripoti ya uchunguzi kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania. Ripoti hiyo inaweka bayana tofauti kati ya maandamano ya amani yanayotambuliwa kisheria na vitendo vya ghasia vilivyoshuhudiwa siku hiyo.

Kisheria, haki ya kuandamana ipo na inalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hususan kupitia Ibara ya 18 na 20. Hata hivyo, haki hiyo ina mipaka yake, ikiwemo sharti la maandamano kuwa ya amani pamoja na kutoa taarifa (notisi) kwa mamlaka husika, kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio ya Oktoba 29 hayakuzingatia masharti hayo, jambo lililoondoa uhalali wake kisheria.

Zaidi ya hapo, haki ya kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea ni haki ya kikatiba inayolindwa na Ibara ya 5. Hivyo basi, kufanya vurugu siku ya uchaguzi kulikuwa ni kuvunja haki za wananchi wengine waliotaka kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia kwa amani. Badala ya kuwa jukwaa la kutoa maoni kwa njia halali, matukio hayo yaligeuka kuwa kikwazo kwa haki za wengine.

Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman wakati akisoma Muhtasari wa Ripoti ya Tume hiyo, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 23, Aprili, 2026 amesema washiriki wa matukio hayo hawakuwa waandamanaji wa amani, bali walihusika katika vitendo vya ghasia huku wakiwa wamebeba silaha mbalimbali zikiwemo mawe, nondo, mapanga, visu, pamoja na vifaa hatarishi kama vilipuzi na bunduki. Hali hii ni kinyume kabisa na sheria za kitaifa na mikataba ya kimataifa inayoruhusu maandamano ya amani yasiyo na silaha wala vitendo vya taharuki.

Kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 na Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu na Binadamu wa mwaka 1981, maandamano yanapaswa kuwa ya amani, yasiyohatarisha maisha ya watu wala kusababisha uharibifu wa mali. Ripoti inaonyesha kuwa matukio ya Oktoba 29 yalikiuka misingi hiyo kwa kusababisha hofu, uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na kuhatarisha usalama wa wananchi.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa matukio hayo hayakuwa ya bahati mbaya, bali yalipangwa, kuratibiwa na hata kufadhiliwa. Waratibu walitumia mbinu mbalimbali kuwashawishi watu kushiriki, wakiwalenga zaidi vijana, waendesha bodaboda, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wajasiriamali wadogo. Wengine walipewa fedha kidogo kuanzia shilingi elfu 10 hadi elfu 50 au kuahidiwa ajira na maisha bora, jambo lililosababisha baadhi yao kushiriki bila kuelewa madhumuni halisi ya matukio hayo.

Aidha, ilibainika kuwa wahusika wakuu hawakuwepo katika maeneo ya matukio, huku waliokamatwa wengi wakiwa ni wananchi wa kawaida waliovutwa au kushawishiwa kushiriki. Mbinu zilizotumika zilijumuisha kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto mali, kutumia pikipiki kusambaza vurugu na kuanzisha matukio katika maeneo mengi kwa wakati mmoja ili kuvuruga mifumo ya usalama.

Matokeo ya ghasia hizo yalikuwa makubwa na ya kusikitisha. Tume ilibaini kuwa jumla ya watu 518 walipoteza maisha, wengi wao wakiwa raia wa kawaida. Vifo vingi vilitokana na majeraha makubwa, ikiwemo kupigwa risasi, kupoteza damu nyingi na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili. Hali hii imeacha maumivu makubwa kwa familia na jamii, huku pia ikipunguza nguvu kazi ya taifa.

Mbali na vifo, ripoti pia inaonyesha uwepo wa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo matumizi ya nguvu kupita kiasi katika baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na vurugu. Haya ni masuala nyeti yanayohitaji uchunguzi wa kina ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.

Katika enzi ya teknolojia, ripoti pia imebaini kuwa baadhi ya picha na video zilizosambazwa mitandaoni zilikuwa si za kweli, bali zilitengenezwa au kuhaririwa kwa kutumia teknolojia ya akiliunde (AI) ili kupotosha umma. Hali hii inaonyesha umuhimu wa wananchi kuwa makini na taarifa wanazopokea na kuzisambaza.

Kwa ujumla, hitimisho la Tume ni wazi kuwa matukio ya Oktoba 29, 2025 hayakuwa maandamano ya amani, bali yalikuwa ghasia zilizokiuka sheria za kitaifa na viwango vya kimataifa. Hivyo, hayapaswi kulindwa chini ya haki ya maandamano ya amani.

Somo kubwa linalopatikana ni kwamba amani ni jukumu la kila mmoja. Wananchi wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya ushawishi unaoweza kuwapelekea kushiriki vitendo vya vurugu, huku wakilinda haki zao kwa njia halali na za kisheria. Vilevile, kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya haki, uwajibikaji na elimu kwa umma ili kuepuka kurudia matukio kama haya.

Mwisho, wito wa maridhiano, umoja na mshikamano ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Taifa linahitaji kujifunza kutoka yaliyopita na kusonga mbele kwa pamoja, likilinda amani kama tunu kuu ya maendeleo na ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.



 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post