" WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA)WASHIRIKI TAMASHA LA KILIMO JIJINI MBEYA,WAHAMASISHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA)WASHIRIKI TAMASHA LA KILIMO JIJINI MBEYA,WAHAMASISHA NISHATI SAFI YA KUPIKIA





📍 *Iwambi, Mbeya* 


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unashiriki katika tamasha la kilimo linalofanyika katika  viwanja vya Iwambi jijini Mbeya kuanzia tarehe 25 mpaka 29 Aprili 2026, ambapo zaidi ya watu 100,000 wakiwemo vijana kutoka mikoa mbalimbali ya kanda ya nyanda za juu kusini wanatarajiwa kushiriki.


Wakala unatumia jukwaa hilo kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi pamoja na kueleza hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo ya vijijini.


Kupitia banda lake, REA imeonesha bidhaa mbalimbali za nishati safi ya kupikia, ambapo bidhaa kuu zinazohamasishwa ni pamoja na matumizi ya majiko ya umeme, majiko ya gesi pamoja na majiko banifu. Teknolojia hizo zimebainishwa kuwa suluhisho muhimu katika kupunguza matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuboresha afya za watumiaji.


Akifungua rasmi maonesho hayo, Kaimu mkuu wa wilaya ya Mbeya ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Mbarali Mhe. Brig. jen. Maulid Hassan Surumbu, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa hatua hiyo itachangia kulinda afya za jamii pamoja na kuhifadhi mazingira.


Aidha, REA imetumia fursa hiyo kueleza hali ya usambazaji wa umeme vijijini, ikibainisha kuwa vijiji vyote vya Tanzania Bara tayari vimefikiwa na huduma ya umeme. Mafanikio hayo yametajwa kuwa ni hatua kubwa katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa vijijini.


Hata hivyo, REA imeeleza kuwa juhudi zinaendelea sasa katika kupeleka huduma ya umeme katika vitongoji ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo muhimu.


Wananchi wanaotembelea banda la REA wamepata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia, gharama zake na namna ya kuipata, huku wakieleza kuridhishwa na jitihada za serikali katika kuboresha upatikanaji wa nishati nchini.


Ushiriki wa REA katika maonesho hayo umeendelea kuwa chachu ya kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia na matumizi ya umeme, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali katika kufikia nishati endelevu kwa wote.


 *Mwisho.*


Post a Comment

Previous Post Next Post