
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tabora, imefanya operesheni maalum katika hifadhi ya msitu wa Igombe River iliyopo wilaya ya Uyui na hifadhi ya msitu wa Nyahua iliyopo wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora.
Katika operesheni hiyo, jumla ya ekari 68 za mashamba ya bangi ziliteketezwa, huku gunia 133 za bangi zikikamatwa na watu saba (7) kutiwa mbaroni.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 30, 2026 katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mamlaka hiyo ipo kwenye operesheni maalum ya kuteketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini.
Amesema hatua hiyo inakuja kufuatia kupungua kwa dawa za kulevya za viwandani, hivyo juhudi zimeelekezwa zaidi katika kudhibiti uzalishaji wa ndani.
“Sasa hivi tuko kwenye kampeni maalum kuhakikisha tunateketeza dawa za kulevya zinazozalishwa nchini baada ya dawa za viwandani kupungua,” amesema Lyimo.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha mamlaka hiyo kuanzisha ofisi za DCEA Kanda ya Magharibi yenye makao yake makuu mkoani Tabora, hatua aliyosema imeongeza ufanisi na kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Sambamba na hilo, Lyimo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano uliotolewa katika kufanikisha operesheni hiyo iliyowezesha kukamatwa na kuteketezwa kwa bangi iliyokuwa ikilimwa ndani ya mapori na hifadhi.
Amesisitiza kuwa mamlaka hiyo haitavumilia vitendo vya uhalifu vinavyohusiana na dawa za kulevya na itaendelea kufanya operesheni endelevu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hatutakubali uhalifu huu uendelee. Tutahakikisha tunafanya operesheni endelevu na kuchukua hatua kali kwa wote wanaojihusisha na kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya ndani na nje ya mapori,” amesisitiza Lyimo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Paul Chacha, ameipongeza DCEA kwa kazi kubwa ya kudhibiti dawa za kulevya inayoendelea mkoani humo.
Aidha, amewaagiza askari wa TFS kuweka kambi katika mapori na maeneo ya hifadhi ili kudhibiti na kumaliza kabisa tatizo la kilimo cha bangi katika Mkoa wa Tabora.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment