" SERIKALI YAFUNGA RASMI KAMBI YA NDUTA: WAKIMBIZI 165,394 KUREJEA BURUNDI

SERIKALI YAFUNGA RASMI KAMBI YA NDUTA: WAKIMBIZI 165,394 KUREJEA BURUNDI

 

Kigoma - Kambi ya Wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo, mkoani Kigoma, iliyokuwa inahifadhi jumla ya wakimbizi 165,394 kutoka nchini Burundi, imefungwa rasmi.


Akizungumza wakati wa ufungaji huo, Aprili 30, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobass Katambi, amesema uamuzi huo umetekelezwa ikiwa ni sehemu ya Serikali kuongeza kasi ya urejeshaji wa wakimbizi nchini kwao kwa hiari. Hatua hii inafuatia makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa 26 wa pande tatu, kati ya Serikali ya Tanzania, Burundi, na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) , uliofanyika tarehe 28 Novemba 2025, Jijini Dar es Salaam


Akifunga kambi hiyo Waziri Katambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake uliowezesha maelfu ya wakimbizi kupata suluhisho la kudumu kwa kurejea kwao kwa amani.


”Ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi na umahili wake katika usimamizi wa uhifadhi wa Wakimbizi na kuendelea kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutekeleza majukumu yake vema na hata kufikia mafanikio haya ya kuwapa maelfu ya Wakimbizi suluhisho la kudumu kwa kurejea nchini kwao kwa hiari yao,” amesema Waziri Katambi
Aidha, aliwapongeza wananchi wa Mkoa wa Kigoma, hususan wa Wilaya ya Kibondo, kwa ukarimu wao mkubwa wa kutoa ardhi kwa miaka mingi ili kuhifadhi wakimbizi hao.


”Ninawapongeza na kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Kigoma, hususan Wilaya ya Kibondo, pamoja na Watanzania kwa ukarimu na uvumilivu mkubwa mlioonesha kipindi chote cha kuwahifadhi wakimbizi.Mliruhusu ardhi yenu kutumika kama kambi ya wakimbizi, na mkawakaribisha kwa moyo mkunjufu. Ukarimu huu ni wa kipekee, na shukrani hizi ziwafikie wote mlioguswa kupitia jukumu hili." alisema Waziri Katambi.


Pamoja na shukurani hizo, Waziri Katambi alisema Serikali imesikitishwa na tukio la tarehe 14 Aprili, 2026, ambapo wakimbizi zaidi ya 9,000 waliingia kambini kwa fujo baada ya huduma za msingi kusitishwa.

”Serikali ya Tanzania imesikitishwa na kitendo cha wakimbizi zaidi ya 9000 kurejea kwa fujo,kitendo hicho hakijawahi kutokea popote tangu nchi ya Tanzania ianze kupokea wakimbizi.Serikali ilikuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua lakini kwa busara na uhusiano mzuri baina ya nchi zetu mbili tuliona ni ndugu zetu na tukawasaidia na kuwaratibu kurudi nyumbani kwao kwa amani na upendo” alisema Katambi
Waziri Katambi ametoa wito kwa wakimbizi waliosalia katika Kambi ya Nyalugusu,wasifanye mchezo huo usio wa kiungwana uliofanywa na wakimbizi wa Nduta.


Amewataka kila mmoja awepo siku aliyopangiwa kurejea ili kuepusha madhara ya kibinadamu yanayoweza kutokea kutokana na dharura inayotengenezwa kwa makusudi kwenye msafara wa mwisho wa kurejea nchini kwao.


Amewatahadharisha wazi ikitokea tena wakimbizi kuingia kambini kwa fujo baada ya msafara wa mwisho, Serikali itatafsiri kuwa ni watoro na hatua za kisheria zitachukuliwa.


”Tunawapenda sana raia wa Burundi. Ni majirani zetu, na nchi zetu zina uhusiano na ushirikiano wa kihistoria. Hatuoni tija wala busara ya kikundi kidogo kinachotengeneza matukio yenye kuleta taharuki katika hifadhi na kuchafua kwa makusudi taswira ya nchi yetu ili kupata huruma ya kimataifa,wakati kuna maelfu ya Wananchi wa Burundi wanaishi kwa amani waliopo Tanzania kihalali kama wafanyabiashara, wafanyakazi, vibarua, wanafunzi na wawekezaji.”aliongeza Waziri Katambi

Post a Comment

Previous Post Next Post