" WAZIRI MKUU AVITAKA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUWA MACHO DHIDI YA WAVUNJA AMANI

WAZIRI MKUU AVITAKA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUWA MACHO DHIDI YA WAVUNJA AMANI

 


Na mwandishi wetu

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho dhidi ya vitendo vinavyolenga kuvuruga amani ya nchi huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia usalama wa wananchi na mali zao.

“Kuweni macho na njama za aina hii, shughulikeni na waovu wa aina hii. Mliweza lile la Kibiti, mliweza lile la Amboni na mambo mengine mengi mmeweza. Kuweni macho kuhakikisha michezo ya aina hiyo haifanikiwi huku mkihakikisha usalama wa raia wetu na mali zao unaendelea kulindwa,” amesema Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumamosi, Mei 23, 2026 alipozungumza na wananchi wa Manispaa ya Iringa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Kichangani mkoani Iringa.

Amesema amani ni msingi wa maendeleo ya Taifa na kwamba Watanzania wanapaswa kuendelea kulinda mshikamano wa kitaifa na kukataa vitendo vya uchochezi vinavyoweza kusababisha migawanyiko ya kisiasa, kidini au kijamii.

“Amani ni msingi wa maendeleo ya taifa letu. Kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama na yenye mshikamano,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema zipo njama mbalimbali zinazolenga kuwagombanisha Watanzania kupitia siasa, dini na taarifa za upotoshaji huku akiwataka wananchi kuwa makini na watu wanaowachochea kufanya vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi.

“Tupuuze na wala tusiwe na ushirika na mtu anayekutuma kuvunja amani wakati yeye hayupo hapo na anajua yeye hataathirika,” amesema.

Kadhalika, Dkt. Mwigulu amesema baadhi ya matukio yanayoendelea kujitokeza nchini yakiwemo madai ya watu kujiteka au kushambuliwa yanapaswa kutazamwa kwa umakini mkubwa kwa kuwa baadhi yake yanaweza kuwa sehemu ya njama za kuwagawa Watanzania na kuichonganisha Serikali na wananchi wake.

“Hizi ni ajenda maalum. Hii ni michezo ambayo inalenga kutengeneza hasira na kuwafanya watu wachukiane,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imejikita zaidi katika kutatua changamoto za wananchi na kusukuma maendeleo badala ya kuendelea kujadili siasa za uchaguzi muda mfupi baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

“Taifa linapotakiwa kupiga hatua, tujadili namna ya kutatua kero za wananchi badala ya kutumia muda mwingi kujadili uchaguzi,” amesema.

Amesema yeye binafsi ameendelea kufanya ziara mbalimbali za kusikiliza wananchi, kupokea changamoto zao na kuhakikisha Serikali inazitatua kwa wakati ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo.

“Watu wanahitaji kusikilizwa, wanahitaji kutatuliwa changamoto zao na wanahitaji maendeleo. Hiyo ndiyo kazi ambayo Serikali imepewa na wananchi,” amesema.

Aidha, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa mshikamano na uvumilivu wa kidini na kijamii barani Afrika kutokana na misingi iliyoasisiwa na viongozi waasisi wa Taifa.

“Hii ndiyo nchi ambayo Mungu ametupatia na Baba wa Taifa ameturithisha. Tukatae vibaraka wanaotaka kuligawa Taifa letu,” amesema.

Waziri Mkuu pia amewaomba viongozi wa dini, wazee wa mila, viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na uzalendo ili taifa liendelee kuwa salama na lenye umoja.

Post a Comment

Previous Post Next Post