" ZIARA YA VIONGOZI WA SENETI MKOA WA SHINYANGA YAENDELEA, WANACHUO WAASWA KUWA WAZALENDO NA KUCHANGAMKIA FURSA

ZIARA YA VIONGOZI WA SENETI MKOA WA SHINYANGA YAENDELEA, WANACHUO WAASWA KUWA WAZALENDO NA KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Ziara ya viongozi wa Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Shinyanga imeendelea leo kwa kutembelea Chuo cha Serikali za Mitaa kilichopo mjini Shinyanga pamoja na Chuo cha Ualimu SHYCOM, ambapo viongozi hao wametoa elimu mbalimbali kwa wanachuo kuhusu uongozi, uzalendo, fursa za maendeleo na wajibu wa vijana katika jamii.


Viongozi ambao wameshiriki katika ziara hiyo ni Mwenyekiti wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Jackson Aloyce Mwizarubi, Katibu wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Lukomanga Jinyage Jiboli pamoja na Katibu Hamasa wa Seneti, Sharon Callist Mathias.

Akizungumza na wanachuo hao, Mwenyekiti wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Jackson Aloyce Mwizarubi, amewataka vijana kutumia vizuri muda wao wa masomo kwa kujijenga kitaaluma na kiuongozi ili waweze kuwa sehemu ya maendeleo ya taifa.

“Nyinyi ndiyo nguvu ya taifa la kesho. Tumia vizuri nafasi mliyoipata ya elimu, jengeni nidhamu, muwe wabunifu na msiogope kutumia ujuzi wenu kujitengenezea ajira,” amesema Mwizarubi.

Kwa upande wake, Katibu wa Seneti Mkoa wa Shinyanga Lukomanga Jinyage Jiboli, amesisitiza umuhimu wa amani, mshikamano na uzalendo kwa vijana wa vyuo, akiwataka kuwa mfano bora katika jamii.

“Amani ya nchi yetu ni msingi wa maendeleo yetu. Vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuilinda na kuhakikisha tunaishi kwa upendo, mshikamano na kuheshimu taratibu zilizopo,” amesema Jiboli.

Naye Katibu Hamasa wa Seneti Mkoa wa Shinyanga, Sharon Callist Mathias, amewahamasisha wanachuo kujiamini, kushiriki katika shughuli za maendeleo pamoja na kutumia vyema fursa zinazopatikana kupitia elimu na uongozi.

“Msikubali kurudishwa nyuma na changamoto. Chuo ni sehemu ya kujifunza maisha, kujenga uwezo na kujiandaa na mustakabali wenu. Changamkieni fursa zinazowazunguka,” amesema Sharon.

Baadhi ya wanachuo waliohudhuria mikutano hiyo wamewashukuru viongozi wa Seneti kwa kuwafikia na kutoa elimu yenye manufaa kwa vijana, huku wakiahidi kuwa wazalendo, kuzingatia masomo yao na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa kupitia Seneti.

Aidha, viongozi hao wamewahimiza wanachuo wote kuendelea kutembelea ukurasa rasmi wa Instagram wa Seneti Mkoa wa Shinyanga ili kupata taarifa mbalimbali, matangazo na shughuli zinazoendelea kufanywa na Seneti hiyo.

Ziara ya viongozi wa Seneti Mkoa wa Shinyanga inaendelea katika vyuo mbalimbali mkoani humo ikiwa ni sehemu ya mpango wa kutembelea vyuo 17 kwa lengo la kuimarisha uongozi wa wanafunzi, kutoa elimu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wanachuo.

Mwenyekiti wa Seneti Mkoa wa Shinyanga, Jackson Aloyce Mwizarubi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Chuo cha Serikali za Mitaa, mjini Shinyanga.



Post a Comment

Previous Post Next Post