Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuhakikisha sekta binafsi, hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), wanakuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa taifa.
Waziri Kapinga aliyasema hayo Mei 7, 2026, wakati wa maadhimisho ya Europe Day yaliyofanyika jijini Dar es Salaam chini ya kaulimbiu “Gateway to Growth”, ambapo viongozi mbalimbali, mabalozi, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa walishiriki.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Kapinga alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya umeendelea kukua kwa zaidi ya miaka 50 kutoka ushirikiano wa maendeleo hadi kuwa ushirikiano mpana unaojumuisha biashara, uwekezaji, miundombinu na ukuaji wa sekta binafsi.
Ameeleza kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuweka mazingira bora ya biashara, kuongeza ushindani wa viwanda na kuvutia wawekezaji.
“Tunataka kuondoka zaidi kwenye utegemezi wa misaada na kuelekea kwenye biashara, uwekezaji na ujenzi wa mifumo ya uzalishaji yenye kuongeza thamani ndani ya uchumi wetu”.
Alisema Tanzania inanufaika na ushirikiano huo kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo uchumi wa kijani, miundombinu, mifumo ya kidijitali, uchumi wa buluu, nishati pamoja na maendeleo ya biashara na viwanda.
Aidha, Waziri huyo alisema Tanzania ipo katika nafasi nzuri kimkakati kutokana na eneo lake, masoko ya kikanda, ongezeko la watu, rasilimali zilizopo na ukuaji wa sekta ya viwanda, hali inayofanya nchi kuwa lango muhimu la biashara kwa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.
Katika hotuba yake, Waziri Kapinga aliwatambua wafanyabiashara wadogo na wa kati kuwa msingi muhimu wa uchumi kwa kuwa wanatoa ajira, kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na kufungua fursa kwa vijana na wanawake.
Alisema serikali itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuhakikisha biashara hizo zinapata mitaji, masoko, teknolojia na mazingira rafiki yatakayowasaidia kukua na kushindana kimataifa.
“SMEs si sehemu ya pembeni ya uchumi wetu, bali ndiyo moyo wa uchumi. Ukuaji wa kweli lazima uwafikie wananchi kupitia biashara na uwekezaji wenye matokeo.”
Waziri Kapinga pia ameupongeza Umoja wa Ulaya pamoja na nchi wanachama wake kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo na biashara.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau, alisema Umoja wa Ulaya unaendelea kuamini katika ushirikiano wa kimataifa unaojengwa juu ya amani, demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Balozi Grau alisema kupitia mpango wa Global Gateway, Umoja wa Ulaya unaendelea kuwekeza katika miundombinu, nishati, biashara, uchumi na maendeleo ya watu ili kusaidia ukuaji wa uchumi jumuishi nchini Tanzania.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa viongozi hao kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya ili kuongeza biashara, uwekezaji na fursa za maendeleo kwa wananchi wa pande zote mbili.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment