" FAXON MBYEMEIRE AWAONYA WAKULIMA: KAHAWA BORA NDIYO TIKETI YA BEI NZURI

FAXON MBYEMEIRE AWAONYA WAKULIMA: KAHAWA BORA NDIYO TIKETI YA BEI NZURI

Na Lydia Lugakila, Misalaba Media

Kagera

Wakati maandalizi ya msimu wa kahawa wa mwaka 2026/2027 yakianza kushika kasi katika wilaya za Karagwe na Kyerwa Mkoani Kagera , Mwenyekiti wa Bodi ya KDCU Ltd, Faxon Mbyemeire, ametoa wito kwa wakulima wa zao hilo kuzingatia ubora katika kila hatua ya uzalishaji ili kulinda sifa ya kahawa ya Kagera na kuhakikisha wanapata bei nzuri katika soko.

Mbyemeire amesema ubora wa kahawa ndiyo nguzo kuu inayowavutia wanunuzi na kuongeza thamani ya zao hilo katika masoko ya ndani na nje ya nchi, akionya kuwa uzembe katika uvunaji na uchakataji unaweza kuathiri sifa ya kahawa ya Kagera ambayo imejijengea heshima kwa miaka mingi.

“Je, ni busara kuharibu sifa ya kahawa yetu na kuchafua soko? Je, ni busara kupoteza wanunuzi na kuwakatisha tamaa wakati wanatupa bei nzuri?” alihoji.

Akizungumza kupitia chombo cha habari cha ushirika huo kilichopo wilayani Karagwe, Mbyemeire alisema wakulima ambao tayari wameanza kuvuna wanapaswa kuhakikisha wanachuma kahawa iliyoiva pekee na kuepuka kuchanganya matunda mabichi na yaliyoiva, hali inayoweza kushusha ubora wa kahawa na kuathiri bei yake sokoni.

Alisisitiza kuwa kahawa inapaswa kukaushwa kwa kiwango kinachokubalika, kupepetwa vizuri na kuondolewa uchafu wote kabla ya kuwasilishwa katika vyama vya msingi vya ushirika.

Kwa mujibu wa Mbyemeire, hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha kahawa inayofikishwa sokoni inakidhi viwango vinavyotakiwa na wanunuzi, jambo linalochangia kuongeza ushindani wa kahawa ya Kagera katika soko la dunia.

Aidha, amewataka wakulima kuhakikisha kahawa yote inayopelekwa katika vyama vya msingi inaambatana na taarifa sahihi za mkulima, chama husika na wilaya anayotoka ili kurahisisha maandalizi ya mnada na kuimarisha uwazi katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo.

Kwa wakulima ambao bado hawajaanza kuvuna, Mbyemeire amewashauri kusubiri kahawa ikomae na kuiva kikamilifu kabla ya kuichuma, akieleza kuwa uvunaji wa kahawa mbichi husababisha kupungua kwa ubora na thamani ya mazao hayo.

Sambamba na hilo, amekemea tabia ya baadhi ya wakulima ya kuvundika kahawa baada ya kuvuna, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaharibu ubora wa mazao na vinaweza kusababisha hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Mbyemeire amesema mafanikio ya sekta ya kahawa hayaishii kwa mkulima mmoja mmoja pekee, bali yanagusa ustawi wa familia, maendeleo ya jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

“Si busara kuharibu sifa ya kahawa yetu, wala si busara kupoteza maelfu na mamilioni ya fedha yanayoweza kupatikana kupitia zao hili alisema kiongozi huyo".

Ameongeza kuwa Wakulima wote wanapaswa kuzingatia ubora wa kahawa ili kuendelea kuvutia wanunuzi na kuongeza thamani ya zao letu,” alisema.

Amesema kuwa msimu wa kahawa wa mwaka 2026/2027 unapaswa kuwa fursa kwa wakulima kuongeza mapato yao kupitia uzalishaji wa kahawa yenye ubora wa hali ya juu, huku akiwataka kuzingatia maelekezo yote ya kitaalamu yanayotolewa na wataalamu wa zao hilo.

Mwenyekiti huyo amewahimiza wakulima kuifanya kaulimbiu ya msimu huu kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku katika shughuli za uzalishaji wa kahawa.

Kaulimbiu ya msimu wa kahawa wa mwaka 2026/2027 ni: “Kahawa Bora, Bei Bora, Maisha Bora.”

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post