" FCC NA ZFCT ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KULINDA USHINDANI WA HAKI

FCC NA ZFCT ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KULINDA USHINDANI WA HAKI

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Ushindani Halali Zanzibar (ZFCT) limefanya ziara ya mafunzo katika Tume ya Ushindani ya Haki (FCC) kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya ushindani wa biashara, udhibiti wa bidhaa bandia pamoja na usimamizi wa mashauri yanayohusiana na ushindani.

Ziara hiyo iliyofanyika katika ofisi za FCC Juni 10, 2026 Jijini Dar es Salaam, imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa ya haki kwa wadau wote.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa alisema kuwa kubadilishana uzoefu na taasisi za ndani ya nchi ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ushindani na kulinda maslahi ya watumiaji dhidi ya vitendo vinavyokiuka sheria za ushindani na biashara.

Alisema ujumbe wa ZFCT unapata fursa ya kujifunza namna FCC inavyotekeleza majukumu yake ya kudhibiti vitendo vya ushindani usio wa haki, kukabiliana na biashara ya bidhaa bandia pamoja na mifumo ya uchunguzi na uendeshaji wa mashauri mbalimbali yanayofikishwa mbele ya taasisi hiyo.

Kwa upande wake, ujumbe wa ZFCT ukiongozwa na Msajili wa Baraza, Bi. Fatma Yahya alieleza kuridhishwa na mafunzo na uzoefu uliopatikana katika ziara hiyo, ukibainisha kuwa utaisaidia taasisi hiyo kuimarisha utendaji wake katika kushughulikia rufaa na mashauri yanayohusiana na ushindani wa biashara Zanzibar.

ZFCT ni chombo kinachoshughulikia mashauri na rufaa zinazotokana na maamuzi ya mamlaka za ushindani, ambapo wadau wasiokubaliana na maamuzi yaliyotolewa huwasilisha kesi zao kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Ziara hiyo pia ilitoa nafasi kwa wataalamu kutoka pande zote mbili kujadiliana changamoto na fursa zilizopo katika usimamizi wa ushindani wa biashara, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kuimarisha utekelezaji wa sheria zinazolinda ushindani wa haki katika soko.

Post a Comment

Previous Post Next Post