Shirika la Viwango Tanzania limeandaa Jukwaa la Biashara la Viwango (Viwango Business Forum) litakalofanyika Juni 5, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, likiwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 1975 na kuanza utekelezaji wake mwaka 1976.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Bi.Deborah Haule Afisa Masoko Mwandamizi amesema jukwaa hilo linalenga kuwakutanisha wadau kutoka sekta za viwanda, biashara, huduma, taasisi za umma na binafsi pamoja na wataalamu wa ubora kwa lengo la kujadili nafasi ya viwango katika kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za Tanzania.
"Washiriki watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu, kujifunza kuhusu masuala ya ubora na usalama wa bidhaa na huduma, pamoja na kujadili namna viwango vinavyoweza kusaidia kufungua masoko ya ndani, kikanda na kimataifa". Amesema
Amesema jukwaa hilo la mwaka huu pia limeunganishwa na utoaji wa Tuzo za Taifa za Ubora (National Quality Award) kwa mwaka 2025/2026, ambazo hutolewa kwa taasisi, kampuni na watu binafsi waliodhihirisha matumizi bora ya viwango na mifumo ya ubora katika shughuli zao.
Vilevile Siku ya Chakula Salama Duniani itaadhimishwa kupitia jukwaa hilo pia.
Aidha, amesema kupitia jukwaa hilo, TBS inalenga kuendelea kuhamasisha matumizi ya viwango, kukuza utamaduni wa ubora na usalama, pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali za kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda, biashara na huduma zenye ubora wa kimataifa.

Post a Comment