Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo kwa upande wa Zanzibar, Ismail Jussa, amemkosoa vikali Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, kufuatia kauli zake alizozitoa hivi karibuni akidai kuwa mwasisi na kiongozi mkuu wa zamani wa ACT, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, alifariki dunia akiwa na majuto ya kujiunga na chama hicho.
Jussa amezitaja kauli hizo kuwa ni za uzushi, uwongo na siasa za kijinga za kilaghai ambazo zinalenga kupotosha ukweli wa kihistoria kwa maslahi mepesi ya kisiasa.
Amesisitiza kuwa Maalim Seif alikuwa kiongozi shupavu, mnyofu na aliyethubutu kufanya maamuzi makubwa tangu zama za Mwalimu Julius Nyerere, na kamwe asingeweza kuficha msimamo au maamuzi yake kama angekuwa na majuto yoyote juu ya uwepo wake ndani ya ACT Wazalendo.
Katika kudadisi ukweli wa mambo, Jussa amehoji sababu za madai hayo kuibuliwa sasa baada ya miaka kadhaa tangu kiongozi huyo aondoke duniani, akitilia shaka ukaribu wowote wa maana uliokuwepo kati ya Mnyika na Maalim Seif enzi za uhai wake. Kiongozi huyo wa ACT ameweka wazi kuwa CHADEMA imekuwa na tabia ya kuendesha siasa za maigizo na utapeli ambapo viongozi wake hubadilika kutokana na maeneo wanayotembelea kwa kuvaa uhusika usio wa kwao ili tu kuwaridhisha watu wa eneo husika.
Jussa ametoa mfano wa viongozi hao kwenda maeneo kama Kilwa wakiwa wamevaa vibaraghashia na kuzungumza maneno ya kuigiza ukaribu, jambo linalothibitisha kuwa hawana misimamo inayosimamia kile wanachokiamini bali wanasema yale ambayo wasikilizaji wanapenda kuyasikia kwa lengo la kujitafutia uungwaji mkono wa bei rahisi.
Msimamo huo thabiti wa Jussa unaanika wazi historia ya CHADEMA ambayo imejaa siasa za vigeugeu, ambapo amewakumbusha jinsi walivyokuwa na kawaida ya kuwatukana na kuwashushia heshima viongozi wenzao wa upinzani, lakini kesho yake wanapowaona wana nguvu wanabadilika na kuwakaribisha kwa vigelegele.
Amewataka viongozi wa chama hicho kuacha tabia ya kujifanya wako karibu na watu kwa kuwatia maneno ya uwongo mdomoni na hata kufikia hatua ya kwenda kupiga dua kwenye makaburi ya viongozi waliotangulia mbele ya haki wakidhani kuwa usanii huo utawafanya wakubalike kwa wananchi.
Ameweka wazi kuwa tabia hizo za kilaghai hazitafanikiwa kile wanachokidhamiria, na kama wanafikiri kuwa mbinu hizo za kisiasa zitakibomoa au kukidhoofisha chama cha ACT Wazalendo, basi wanajidanganya kwa kiasi kikubwa.
Jussa amesisitiza kuwa ACT Wazalendo inaendelea kuimarika kwa kasi kubwa nchini na imezidi kuweka matumaini mapya na ya kweli kwa Watanzania wanaotamani mabadiliko yenye tija na misingi thabiti.
Ameongeza kuwa CHADEMA wanapaswa kukubali ukweli huo badala ya kuendekeza hofu inayowapelekea kumzulia uwongo marehemu ambaye hawezi kusimama na kujitetea.
Amewataka viongozi wa chama hicho kurejea kwenye siasa za kistaarabu na zilizonyooka, na waache kueneza kauli za uwongo na za kijinga kuhusu Maalim Seif kujutia hatua yake ya kuingia ACT, akibainisha kuwa siasa za namna hiyo hazina tija katika ustawi wa demokrasia na ujenzi wa taifa.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment