" KIKAO CHA KAMATI YA UTEKELEZAJI CHA KIKANUNI CHA JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA MPANDA

KIKAO CHA KAMATI YA UTEKELEZAJI CHA KIKANUNI CHA JUMUIYA YA WAZAZI WILAYA YA MPANDA

Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda imeendelea kuonyesha dhamira thabiti ya kuimarisha maendeleo ya kijamii, kielimu, kiuchumi na kisiasa kupitia kikao chake cha Kamati ya Utekelezaji cha Kikanuni kilichofanyika tarehe 04 Juni 2026. Kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuendeleza uhai wa jumuiya, kuongeza ushiriki wa wanachama, kuimarisha miradi ya maendeleo pamoja na maandalizi ya shughuli muhimu za kitaifa.

Katika ajenda ya kwanza, kikao kilijikita katika kujadili uhai wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda. Wajumbe walisisitiza kuwa nguvu ya jumuiya hutegemea ushiriki wa wanachama wake katika kutekeleza wajibu wao wa msingi, ikiwemo ulipaji wa ada za uanachama. Kamati ya utekelezaji ilihimiza viongozi wa matawi, kata na wanachama wote kuhakikisha kila mmoja analipia ada kwa wakati ili kuendeleza uhai na ufanisi wa jumuiya katika ngazi zote.

Kikao hicho pia kilijadili suala la usajili wa wanachama kwa lengo la kuongeza idadi ya wanachama wa Jumuiya ya Wazazi. Wajumbe walikubaliana kuwa ni muhimu kutoa elimu na hamasa kwa wanachama waliopo pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali ili kuwavutia wanachama wapya kujiunga na jumuiya.

Aidha, ilielezwa kuwa maafisa wa jumuiya na maafisa wa TEHAMA watapita katika matawi na kata kutoa elimu kuhusu namna ya kujiunga na kulipia ada za uanachama kwa kutumia simu, mawakala na benki. Hatua hiyo inalenga kurahisisha huduma za uanachama na kuongeza uwazi katika mfumo wa malipo.

Moja ya ajenda zilizochukua nafasi kubwa katika kikao hicho ilikuwa ni mjadala kuhusu Shule ya Ufundi Milala iliyopo Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi. Wajumbe walieleza masikitiko yao kuwa shule hiyo, ambayo ni shule kongwe inayofahamika kwa wananchi wengi, imekuwa haifanyi kazi kwa zaidi ya miaka mitano.

Kamati iliona kuna haja ya kuipima shule hiyo, kuboresha miundombinu yake na kupanga vizuri maeneo yake ili iweze kuanza tena kutoa mafunzo ya ufundi na elimu mbalimbali kwa vijana na jamii.

Kikao pia kilibaini kuwa shule hiyo haina hati miliki ya eneo lake, jambo ambalo limekuwa chanzo cha sintofahamu kwa baadhi ya watu. Hivyo, kamati ilisisitiza umuhimu wa kupambana kwa kadri ya uwezo kuhakikisha shule hiyo inapata hati miliki ili kulinda mali ya jumuiya na kuondoa uvumi usio na msingi.

Wajumbe waliweka wazi kuwa sababu kubwa ya shule hiyo kutofanya kazi si mgogoro wa kanisa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali ni ukosefu wa fedha kiasi cha Tsh. 2,333,000/= kwa ajili ya upimaji wa eneo, upangaji wa maeneo na ukosefu wa mshikamano wa pamoja katika kuendeleza mradi huo wa kimkakati.

Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda ilitoa wito kwa wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na shule hiyo kujitokeza kusaidia, hususan katika kugharamia upimaji wa eneo na kuboresha mazingira ya shule kwa kushirikiana na viongozi wa jumuiya na Chama Cha Mapinduzi.

Kamati ya utekelezaji ilijadili pia umuhimu wa miradi ya kiuchumi kwa ajili ya kuiwezesha Jumuiya ya Wazazi kuwa na uwezo wa kujitegemea kifedha. Wajumbe walikubaliana kuwa miradi hiyo itasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa vikao, ziara na shughuli nyingine za jumuiya.

Sambamba na hilo, wanachama katika matawi na kata walihimizwa kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayopanua wigo wa maendeleo ya jumuiya badala ya kutegemea michango pekee.

Kikao kilipokea taarifa ya tathmini ya Maadhimisho ya Sherehe ya Wiki ya Wazazi Wilaya ya Mpanda yaliyofanyika tarehe 07 Mei 2026 katika Kata ya Mtapenda, eneo la Hospitali ya Halmashauri ya Nsimbo.

Wajumbe walieleza kuwa maadhimisho hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa chini ya mgeni rasmi Ndugu Evarist Simon Mnyele, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Katavi. Shughuli kuu zilizofanyika ni pamoja na kutoa misaada kwa wagonjwa na kupanda miti ya matunda na kivuli.

Viongozi wa Chama na Serikali walishiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, jambo lililotajwa kuimarisha ushirikiano kati ya Jumuiya ya Wazazi, Chama Cha Mapinduzi na Serikali.

Kamati ya utekelezaji ilijadili maandalizi ya Baraza la Kikanuni la Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda litakalofanyika tarehe 24/06/2026. Baraza hilo linafanyika kwa mujibu wa taratibu za kikanuni zinazotaka jumuiya kufanya baraza katika juma la mwisho la mwezi wa sita.

Kupitia kikao hicho, viongozi walisisitiza umuhimu wa kufanya ziara katika matawi na kata kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu malezi, mazingira na kuimarisha uhai wa jumuiya ndani ya Wilaya ya Mpanda.

Ajenda nyingine muhimu ilikuwa ni maandalizi ya ushiriki wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda katika Maadhimisho ya Sherehe ya Wiki ya Wazazi Kitaifa yatakayofanyika Mkoa wa Mwanza kuanzia tarehe 30/06/2026 hadi 04/07/2026.

Kamati ilieleza kuwa ushiriki katika maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuonyesha umoja, mshikamano na kuimarisha mahusiano ya jumuiya na Chama Cha Mapinduzi.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha wajumbe wote kuanza kutoa taarifa kwa wanachama kuhusu umuhimu wa kushiriki maadhimisho hayo ya kitaifa.

Aidha, alisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni nguvu na nguzo kubwa ya maendeleo na mafanikio ya jumuiya na chama. Aliwataka wanachama kuona ushiriki wao katika maadhimisho hayo kama ishara ya upendo, amani na kujenga Chama Cha Mapinduzi.

Kikao cha Kamati ya Utekelezaji cha Kikanuni cha Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda kilionyesha dhamira kubwa ya viongozi na wanachama katika kuimarisha jumuiya, kuendeleza miradi ya maendeleo, kukuza elimu na kuongeza mshikamano ndani ya chama na jamii kwa ujumla.

Kauli mbiu iliyotolewa katika kikao hicho ilikuwa:

“SAMAKI MKUNJE ANGALI MBICHI”

Kauli hiyo ilitumika kuhimiza malezi bora, nidhamu na kuwekeza katika maendeleo ya kizazi cha sasa kwa manufaa ya taifa la kesho.

Viongozi wa chama baada ya kuwasili.




Ndugu Pius M. Buzumalle, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, alishiriki kikamilifu kikao cha kikanuni cha Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda kilichofanyika tarehe 04 Juni 2026.

Katika kikao hicho cha kawaida kinachofanyika kila baada ya miezi mitatu, Mwenyekiti Buzumalle alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya uongozi. Alieleza kuwa uwajibikaji mzuri ndiyo ngao na msingi wa mafanikio katika kutekeleza majukumu tuliyokabidhiwa, huku akiwahimiza viongozi na wajumbe wote kutimiza wajibu wao kwa weledi, umoja na mshikamano kwa maendeleo ya Jumuiya na Chama kwa ujumla.

Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, akizungumza na kusalimia wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji wakati wa kikao cha kikanuni cha Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda.

Katika salamu zake za ukaribisho, aliwapongeza wajumbe kwa kujitokeza kushiriki kikao hicho na kusisitiza kuwa umoja na mshikamano ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya ya Wazazi. Aidha, aliwahimiza viongozi na wanachama kuendelea kushirikiana, kuheshimiana na kutekeleza wajibu wao kwa bidii ili kuimarisha maendeleo ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda na Chama kwa ujumla.

Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali walishiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Sherehe ya Wiki ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, wakionesha mfano wa umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya jamii.

Ushiriki wao ulidhihirisha dhamira ya pamoja ya kuimarisha Jumuiya ya Wazazi na kuendeleza maadili ya kujitolea, upendo na uwajibikaji. Umoja na mshikamano uliotawala katika maadhimisho hayo uliendelea kuwa chachu ya mafanikio na maendeleo ya Jumuiya ya Wazazi pamoja na Chama kwa ujumla.

 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post