Na John Bukuku, Dar es Salaam
Msajili wa Baraza la Famasi, Mfamasia Magige, amesema kuwa kuanzishwa kwa Ofisi za Kanda sita za Baraza hilo kumeongeza ufanisi katika usajili, usimamizi na udhibiti wa taaluma ya famasi pamoja na huduma za dawa nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wahariri na waandishi wa habari iliyofanyika katika Maabara Kuu ya Serikali Mabibo jijini Dar es Salaam, Julai 1, 2026, Mfamasia Magige alisema hatua hiyo imewezesha Baraza kuwafikia wadau kwa urahisi zaidi na kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo ya utoaji huduma za dawa katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema Ofisi za Kanda za Kaskazini, Ziwa, Mashariki, Nyanda za Juu Kusini, Kati na Magharibi zimekuwa sehemu muhimu ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta hiyo, ikiwemo kufuatilia usajili wa wataalamu, vituo vya huduma za dawa na kuhakikisha viwango vya taaluma vinazingatiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Famasi, mwaka 2015 kulikuwa na wanataaluma 1,264 waliosajiliwa, maduka ya dawa 1,116, vyuo vilivyoidhinishwa 519, wafamasia 677, mafundi dawa sanifu 1,250 na mafundi dawa wasaidizi watatu.
Mfamasia Magige amesema hadi mwaka 2026, idadi hiyo imeongezeka ambapo wanataaluma waliosajiliwa wamefikia 4,494, maduka ya dawa 11,245, vyuo vilivyoidhinishwa 1,190, wafamasia 3,792, mafundi dawa sanifu 16,087 na mafundi dawa wasaidizi sita.
Amesema ongezeko hilo ni matokeo ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuimarisha mfumo wa huduma za dawa, huku Baraza likiendelea kuhakikisha wataalamu wanaosajiliwa wanakuwa na uwezo na viwango vinavyokidhi mahitaji ya jamii.
Mfamasia Magige alieleza kuwa Baraza linaendelea kushirikiana kwa karibu na vyuo vikuu kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) katika kuhakikisha programu za mafunzo ya famasi zinakidhi viwango vinavyotakiwa na kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta ya afya nchini.
Alisema ushirikiano huo unalenga kuboresha mitaala, kuimarisha ubora wa mafunzo kwa wanafunzi wa famasi na kuhakikisha wahitimu wanaingia katika soko la ajira wakiwa na uwezo wa kutoa huduma salama na zenye ubora kwa wananchi.
Baraza la Famasi ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoanzishwa kwa Sheria ya Famasi ya mwaka 2011, Sura 311, ikiwa na jukumu la kusimamia na kudhibiti taaluma ya famasi pamoja na kuhakikisha dawa zinatolewa kupitia maeneo yaliyoidhinishwa.
Mfamasia Magige alisema kuwa Baraza linasajili na kusimamia majengo yote yanayohusika na huduma za dawa ikiwemo famasi za jumla, famasi za rejareja na Maduka ya Dawa Muhimu (DLDM), ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na zenye ubora.
Aliongeza kuwa ongezeko la vituo hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya kushirikisha sekta binafsi katika utoaji wa huduma za dawa, hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya huduma hizo.
Mbali na kusajili vituo, Baraza pia linaendelea kusajili na kusimamia wanataaluma wa kada mbalimbali za famasi wakiwemo wafamasia, mafundi dawa sanifu na mafundi dawa wasaidizi, kwa lengo la kuhakikisha wanazingatia maadili na viwango vya taaluma. Katika kutekeleza jukumu hilo, Baraza linatumia Kanuni ya Utendaji (Code of Practice) pamoja na Kanuni ya Maadili ya Wanataaluma wa Famasi kama nyenzo muhimu za kusimamia mwenendo, uwajibikaji na ubora wa huduma zinazotolewa na wataalamu hao. Kanuni hizo zinawaongoza wataalamu kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia maslahi ya afya ya jamii.
Katika kuboresha utoaji huduma, Mfamasia Magige alisema Baraza limeanzisha mifumo ya kidijitali ikiwemo mifumo ya usajili na malipo kwa njia ya kielektroniki pamoja na programu ya simu ya mkononi, hatua inayorahisisha huduma kwa wataalamu na wananchi.
Alisema mifumo hiyo imeongeza ufanisi katika utoaji huduma, ukusanyaji wa mapato na upatikanaji wa taarifa kuhusu vituo vya dawa na wanataaluma waliosajiliwa.
Aidha, Baraza limeendelea kushirikiana na taasisi nyingine za udhibiti ikiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuhakikisha huduma za dawa nchini zinasimamiwa kwa ufanisi na kulinda usalama wa wananchi.
Katika mpango wa Maduka ya Dawa Muhimu (DLDM), Mfamasia Magige alisema Baraza linaendelea kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha wananchi wanapata dawa muhimu kwa njia salama, huku wamiliki wa maduka hayo wakitakiwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia dawa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuepuka madhara ikiwemo usugu wa vimelea dhidi ya dawa, gharama kubwa za matibabu na athari nyingine za kiafya.
Semina hiyo ya wahariri na waandishi wa habari imelenga kuwaongezea uelewa wanahabari kuhusu majukumu ya Baraza la Famasi, usimamizi wa huduma za dawa nchini na nafasi ya vyombo vya habari katika kutoa elimu sahihi kwa jamii.


SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment