" DKT. NCHIMBI AHIMIZA UBUNIFU KWA VIJANA KATIKA SEKTA YA AFYA

DKT. NCHIMBI AHIMIZA UBUNIFU KWA VIJANA KATIKA SEKTA YA AFYA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amehimiza uwapo wa ubunifu wa programu zitakazowaandaa vijana kukabiliana na changamoto za siku zijazo kwa kujiamini.

Dkt. Nchimbi amesema hayo leo wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nne wa kuenzi na kuendeleza Urithi wa Hayati Benjamin William Mkapa na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF), hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.


Katika hotuba yake, Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa vijana ndiyo viongozi wa sekta ya afya wa kesho, watumishi wa afya, na watafiti wajao.


Amefafanua kuwa maisha na uongozi wa Hayati Benjamin Mkapa unatoa mafunzo mengi, hususani katika usimamizi na uendelezaji wa sekta ya afya nchini, kutokana na kutambua kwake nafasi ya afya bora katika maendeleo.

Aidha, amekumbusha kuwa Hayati Mkapa katika awamu yake aliweka mkazo mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI, Malaria, na magonjwa mengine yanayoambukizwa na yasiyo ya kuambukiza.

Makamu wa Rais amewataka viongozi katika sekta ya afya kuelewa uhusiano uliopo kati ya afya na uchumi, siasa, utamaduni, pamoja na muunganiko kati ya mifumo ya afya ya kitaifa na ya kimataifa.

Amewahimiza vijana kutumia kikamilifu fursa zitokanazo na maendeleo ya teknolojia kama akili mnemba, tiba kwa njia ya mtandao, uchambuzi wa takwimu, na teknolojia mpya zitakazoendelea kubadilisha tasnia ya afya.

Katika kuonesha uungaji mkono wa Serikali, Dkt. Nchimbi ameipongeza Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa mchango wake, na kusisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika kukuza elimu ya sayansi, hususan katika taasisi za elimu ya juu kupitia programu mbalimbali.

Pia, amepongeza ushirikiano kati ya Taasisi hiyo na Wizara ya Afya katika kuanzisha jukwaa la vijana kujadili ajenda ya rasilimali watu katika sekta ya afya.

Kutokana na umuhimu wa majadiliano hayo, Makamu wa Rais ameunga mkono azma ya kuubadilisha mkutano huo kutoka mkusanyiko wa mara moja kila baada ya miaka miwili, na kuwa jukwaa kuu la Afrika la fikra za kitaalamu, majadiliano ya sera, ubunifu, na kubadilishana maarifa kuhusu nguvu kazi ya afya, litakalofanyika mara moja kila mwaka.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mlezi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa maendeleo wa kitaifa na kimataifa, wadau wa sekta ya afya, pamoja na wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post