" ECSA- HC YATOA SHILINGI MILIONI 211 KUFANIKISHA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA TANZANIA.

Top News

ECSA- HC YATOA SHILINGI MILIONI 211 KUFANIKISHA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA TANZANIA.




Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Tanzania na wadau mbalimbali, imeandaa kambi maalum ya huduma za madaktari bingwa na bobezi iliyoanza Julai 20 hadi 30 mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Arusha Mount Meru na Hospitali ya Kanda ya Kusini ya Mtwara.


Akizungumza Jijini Arusha kuhusu kambi hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dkt. Ntuli Kapologwe, amesema kambi hizo zinalenga kuwahudumia wananchi wenye mahitaji mbalimbali ya upasuaji na huduma za kitabibu, huku ECSA ikitoa shilingi milioni 211 kufanikisha zoezi hilo.


Amesema kati ya fedha hizo, shilingi milioni 52 zitatumika kununua vifaa tiba, dawa na mahitaji mengine muhimu, huku shilingi milioni 158 zikielekezwa kugharamia wataalamu pamoja na madaktari bingwa na bobezi watakaotoa huduma kwa takribani siku 10.


Dkt. Kapologwe ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wa Wizara ya Afya wakiongozwa na Waziri Mohammed Mchengerwa na Katibu Mkuu Dkt. Grace Maghembe kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika maandalizi ya zoezi hilo na  wadau mbalimbali, wakiwemo mabenki, kwa michango yao iliyowezesha kufanikisha utekelezaji wa kambi hizo.


Amesema mbali na kupunguza maumivu na kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wa huduma za kibingwa, lengo kuu la mpango huo ni kuwawezesha wagonjwa kurejea katika hali yao ya kawaida ili waendelee kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo pamoja na pato la Taifa.


Ameongeza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya programu ya ECSA inayotekelezwa katika nchi mbalimbali, baada ya kufanyika Lesotho na Uganda, huku Tanzania na Malawi zikitekeleza kambi hizo kwa kipindi na tarehe zinazofanana.


Halikadhalika, Dkt. Kapologwe amewataka wananchi wenye uhitaji wa huduma za upasuaji kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo ili warejee katika  katika afya njema na maisha yao ya kawaida.

Post a Comment

Previous Post Next Post