Kutokana na hali ya nchi kuendelea kuwa shwari, Jeshi la Polisi limesema sasa litapokea taarifa za nia ya kufanya mikutano ya kisiasa, hivyo wenye nia hiyo wanatakiwa kuwasilisha taarifa kwa Wakuu wa Polisi Wilaya kama sheria inavyoelekeza.
Taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Polisi mjini Dodoma imefafanua kuwa hali hiyo ya mikutano inatokana na kuendelea kuwepo kwa amani nchini.
Jeshi la Polisi, limewashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kuzingatia maelekezo na kutofuata au kushiriki katika vitendo hivyo vya kihalifu.
"Kitendo cha wananchi kuvikataa vitendo hivyo ndicho kilichowezesha nchi kuwa shwari kwa sasa, ikumbukwe kuwa katika kipindi ambacho nchi ilikuwa ikipitia wakati huo mgumu wa baadhi ya watu kupanga na kuhamasisha uhalifu, Jeshi la Polisi lilikuwa likipokea taarifa kutoka vyama mbalimbali vya siasa na baadhi ya waheshimiwa wabunge waliokuwa wakitoa taarifa za nia ya kufanya mikutano ya hadhara na vikao kwenye majimbo, ambapo jeshi hilo ambalo ndilo lenye mamlaka ya kusimamia usalama katika mikutano hiyo lilikuwa likiwaita na kufanya nao vikao vya kuwashauri kuahirisha kutokana na hali iliyokuwepo wakati huo" ilisema taarifa hiyo.
Aidha Jeshi la Polisi Tanzania limesema linapenda kuwajulisha wananchi na wadau wengine kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, huku likikumbusha kuwa kwa nyakati tofauti jeshi hilo limekuwa likitoa taarifa za kiusalama ikiwepo za baadhi ya watu kupanga na kuhamasisha kufanya vitendo vya kihalifu kwa kutumia maandamano yasiyofuata sheria, kanuni, na taratibu za nchi.
Katika kupanga na kuhamasisha huko, wahusika walikuwa wakielekezana mbinu za kufanikisha malengo yao zikiwemo kuua watu, kuchoma moto shule ili kuleta hofu na taharuki kwa wazazi na walezi, kulipua transfoma za Tanesco, kufunga barabara, na kuwapora askari silaha, mambo ambayo walikuwa wakiyapanga kupitia vikao vya ana kwa ana, kurubuni baadhi ya vijana, na kutumia mitandao ya kijamii kusambaza jumbe mbalimbali na kufanya mikutano kupitia klabu za mitandaoni.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama lilifanikiwa kuwafuatilia kwa karibu na kuwakamata baadhi yao ambapo idadi yao ilitangazwa Julai 9, 2026, na kati yao wameshafikishwa mahakamani kama ilivyotolewa taarifa tarehe 26.7.2026 huku wengine wakiendelea kutafutwa.
Aidha, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa kila mmoja kuendelea kuvikataa na kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya kupanga kutenda uhalifu au kuhamasisha vitendo vya kihalifu ili hatua za haraka zichukuliwe kuvidhibiti kabla ya kukua na kuwa uhalifu, kwani amani na usalama ndiyo mtaji wa kwanza katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment