" MAAFISA USAFIRISHAJI KATA YA NYANDEKWA WAPATIWA ELIMU YA USALAMA BARABARANI

MAAFISA USAFIRISHAJI KATA YA NYANDEKWA WAPATIWA ELIMU YA USALAMA BARABARANI


Maafisa usafirishaji (bodaboda) wa Kata ya Nyandekwa katika Manispaa ya Kahama wamepewa elimu ya usalama barabarani na Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kahama, Mrakibu wa Polisi (SP) Flora Nangawe, aliyekutana nao katika kituo chao kilichopo Nyandekwa.

Akizungumza na madereva hao, SP Nangawe amewataka kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kuvaa vifaa vya kujikinga na hatari, hususan kofia ngumu, pamoja na kuendesha pikipiki kwa mwendo unaokubalika kisheria ili kuepuka ajali.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kusoma katika vyuo vinavyotambulika ili kupata leseni halali ya udereva na kuwaonya kutotumia pikipiki zao kuwafundishia watu wengine kuendesha, akieleza kuwa mafunzo hayo yanapaswa kutolewa na vyuo vya udereva vilivyosajiliwa.

Sambamba na hayo, SP Nangawe amewahimiza kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, pamoja na kuhakikisha vyombo vyao havitumiki katika vitendo vya uhalifu.

Ameeleza kuwa watakaoruhusu pikipiki zao kutumika kwenye uhalifu wanaweza kujikuta wakihusishwa na makosa hayo na, endapo watapatikana na hatia, wanaweza kuhukumiwa kifungo jela pamoja na kulipa faini.

Post a Comment

Previous Post Next Post