
Na John Mapepele, WAF – Kilimanjaro
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini katika utoaji wa huduma za afya nchini. Amesema ushirikiano huo ni msingi ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na unaoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika Hospitali ya Huruma wilayani Rombo Julai 24, 2026 wakati wa uzinduzi wa jengo la huduma za dharura, Mchengerwa amesema ameridhishwa na maandalizi makubwa yanayoendelea ya kuifanya hospitali hiyo kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Alisema hatua hizo zinaonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za afya na kuwafikishia wananchi huduma bora zaidi.
Waziri huyo amesema kuwa kabla ya ziara hiyo alipokea maelekezo mahsusi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya afya na umeendelea kuwa sera ya taifa kwa Serikali zote tangu Uhuru.
Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ili kupunguza changamoto ya umbali wa kufuata matibabu. Alibainisha kuwa lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya kwa urahisi katika maeneo yaliyo karibu na makazi yake.
Akizungumzia maombi yaliyowasilishwa na viongozi wa Hospitali ya Huruma, Waziri Mchengerwa amesema Rombo imepewa kipaumbele katika upatikanaji wa gari la wagonjwa (ambulance). Ameongeza kwamba, uamuzi huo umetokana na mshikamano na juhudi alizoziona kutoka kwa viongozi pamoja na wananchi wa eneo hilo. “Yapo maeneo mengi yenye uhitaji mkubwa, lakini kwa sababu ya mshikamano na juhudi nilizoziona hapa leo, Rombo itaanza kupata ambulance hiyo,” amesema.
Kuhusu ombi la kuiboresha Hospitali ya Huruma kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Waziri amesema Serikali inaunga mkono jitihada hizo na kuwataka viongozi pamoja na wadau kuendelea kukamilisha maeneo yaliyobaki ya ujenzi ili kufanikisha azma hiyo. Aidha, amewataka viongozi wa hospitali na wilaya kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha miundombinu ya afya.
Katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya hospitali hiyo, Mhe. Mchengerwa alitoa mchango binafsi wa shilingi milioni moja kusaidia kukamilisha ujenzi unaoendelea. Pia aliwahimiza wadau wengine kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na sekta binafsi utaendelea kuwa nguzo muhimu katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa ameridhishwa na maendeleo ya miradi mbalimbali ya maendeleo aliyoikagua wilayani Rombo. ikiwepo Kituo cha Forodha cha mpaka wa Tanzania na Kenya cha Holili, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Chuo cha Sayansi ya Afya, Hospitali ya Wilaya ya Rombo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Msingi Kibaoni, ambayo kwa pamoja ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni sita. Ametoa wito kwa wananchi na viongozi kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa na kutunzwa mara itakapokamilika.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment