" MEYA DR NICAS WA MANISPAA KIBAHA ASHIRIKI MKUTANO WA MAMEYA DUNIANI MOROCCO

MEYA DR NICAS WA MANISPAA KIBAHA ASHIRIKI MKUTANO WA MAMEYA DUNIANI MOROCCO



Meya wa Manispaa ya Kibaha Mjini, Dr. Nicas Mawazo, ameshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Mameya Duniani (UCLG World Congress 2026) uliofanyika jijini Tangier, Morocco kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026, uliowakutanisha zaidi ya viongozi 3,000 wa Serikali za mitaa kutoka nchi mbalimbali duniani.



Mkutano huo ni jukwaa kubwa la kimataifa linalowakutanisha mameya na viongozi wa miji kujadili masuala ya maendeleo endelevu ya mijini, huduma za umma, mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji wa miundombinu, kuongeza ajira kwa vijana, namna ya kuhusisha vijana katika uchumi wa Dunia, teknolojia na usafiri wa mijini.

Akizungumzia ushiriki wake, alisema mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu la kuendelea kuona mifumo ya kisasa ya usimamizi wa miji, inayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii na kuimarisha maendeleo ya miji.

Dr. Nicas ambaye ni meya pekee kutoka Tanzania kushiriki tukio hilo, alibainisha kuwa uzoefu alioupata utasaidia kuendelea kuimarisha mipango ya maendeleo ya Manispaa ya Kibaha na Tanzania, hususan katika maeneo ya mipango miji, usafi wa mazingira, huduma za jamii na uwekezaji wa miundombinu..

Mkutano huo unafahamika kama moja ya majukwaa muhimu zaidi duniani kwa kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa miji na kubadilishana mbinu bora za maendeleo ya mijini.

Post a Comment

Previous Post Next Post