" MILIONI 436.7 KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA YA NYAKATO - MTAKUJA, MAJI HOTELI - LYANZUNGU - CHELSEA MANISPAA YA KAHAMA

MILIONI 436.7 KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA YA NYAKATO - MTAKUJA, MAJI HOTELI - LYANZUNGU - CHELSEA MANISPAA YA KAHAMA

 





Mbunge wa jimbo la Kahama Mjini enjamin Ngayiwa kizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Mtakuja - Nyakato unaohusisha mitaro ya maji ya mvua na barabara kwa kiwango cha changarawe utakaogharimu zaidi ya Shilingi milioni 436.




💧Ujenzi wa barabara hizi mbili inajumuisha ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua kuondoa adha ya maji kujaa kwenye makazi ya watu kipindi cha masika.




💧KAHAMA



Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kahama umeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe wenye thamani ya Shilingi milioni 436.7, utakaohusisha ujenzi wa mitaro, makalavati ya kisanduku (box culverts) pamoja na uboreshaji wa barabara katika Manispaa ya Kahama, huku ukitarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu.



Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi huo, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Kahama, Masola Juma, amesema mradi huo unahusisha uboreshaji wa barabara za Nyakato–Mtakuja na Maji Hotel–Chelisi Vyanzungu, ambazo ni miongoni mwa barabara muhimu zinazotumiwa na wananchi wa Manispaa ya Kahama.



Amesema mradi huu unaotekelezwa na mkandarasi Jonta investiment ambaye mkataba wa mradi huo ulisainiwa Juni 16, 2026 na mkandarasi alikabidhiwa eneo la kazi Juni 23, 2026, huku utekelezaji ukianza mara moja.



"Mradi huu una gharama ya jumla ya Shilingi milioni 436.7 na unatekelezwa na kampuni ya Jordan Investment. Tunatarajia kuukamilisha na kuukabidhi Oktoba 21 mwaka huu," amesema Masola.



Amefafanua kuwa kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa takribani kilomita 1.5 za mitaro katika barabara ya Nyakato–Mtakuja, ujenzi wa box culverts nne katika maeneo mbalimbali, ujenzi wa kilomita 4.8 za barabara pamoja na uwekaji wa changarawe katika kilomita mbili.



Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amewataka wahandisi wa TARURA na mkandarasi kuhakikisha kazi zote zinazingatia viwango ili fedha zilizotolewa na Serikali zitoe thamani kwa wananchi.



Ngayiwa amesema changamoto kubwa ya barabara nyingi ndani ya Manispaa ya Kahama imekuwa ni maji ya mvua kupita juu ya barabara kutokana na ukosefu wa mifumo bora ya mitaro.



"Lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunajikita zaidi katika kutengeneza mitaro ili hata mvua zinapokuwa zinanyesha, maji yapate sehemu ya kupita na barabara zibaki imara na zenye kupitika kipindi chote cha masika na kiangazi," amesema.



Amewataka wahandisi wa TARURA kusimamia kwa karibu ubora wa kazi hiyo huku akisisitiza matumizi sahihi ya uwiano wa saruji katika ujenzi wa mitaro.



"Simamieni kazi hii vizuri, Tujiridhishe kuwa mitaro inajengwa kwa viwango vinavyotakiwa. Isije mvua za kwanza zikabeba mitaro tukaanza upya tena," amesisitiza.



Mbunge huyo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya Shilingi milioni 436 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa ni wajibu wa wataalamu kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo.



Ameongeza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inapitisha magari mengi yanayounganisha maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kahama, huku uboreshaji wa barabara ya Chalisi lya nzungu ukitarajiwa kutoa njia mbadala na kupunguza msongamano wa magari katikati ya mji.



Ngayiwa pia ameiagiza TARURA kufanya tathmini ya haraka katika barabara inayoelekea Shule ya Msingi Maila, baada ya kubainika kuwa wanafunzi hukumbwa na changamoto ya kushindwa kufika shuleni kipindi cha mvua.




Meya wa Manispaa ya Kahama, Mataluma Kaniki, amesema utekelezaji wa mradi huo utamaliza changamoto ya mafuriko na uharibifu wa barabara uliokuwa ukiwakabili wananchi kwa miaka mingi.



"Barabara hii ilikuwa kero kubwa sana wakati wa masika, Wananchi walipata shida kubwa na baadhi ya nyumba zilikuwa zikizingirwa na maji, Tunamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha hizi kupitia Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Kaniki.



Amewataka mkandarasi na wahandisi wa TARURA kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua.



Kaniki ameongeza kuwa Manispaa ya Kahama imetenga fedha katika bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ununuzi wa greda, hatua itakayosaidia kupunguza gharama za kukodisha mitambo na kuboresha matengenezo ya barabara za ndani.



Naye mkandarasi wa kampuni ya Jonta Investment, Musa Julius, amesema kampuni yake imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.


"Tunatekeleza ujenzi wa mitaro, makalavati, uwekaji wa changarawe pamoja na kufomu barabara, Kwa sasa hatuna changamoto yoyote ya upatikanaji wa maji, hivyo tunaamini kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa," amesema.



Amemshukuru Mbunge wa Kahama Mjini kwa juhudi zake za kufanikisha upatikanaji wa fedha za mradi huo, akiahidi kuwa kampuni yake itazingatia ubora katika utekelezaji wa kazi.



Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakato, Hussein Mwita, amesema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiteseka kutokana na ubovu wa barabara wakati wa masika.



"Barabara hii ilikuwa korofi sana Mvua ziliponyesha wananchi walishindwa kupita kutoka mtaa huu kwenda mwingine, Leo tunaona utekelezaji unaendelea na tunaamini kero hii itaisha kabisa," amesema.




Amesema uboreshaji wa barabara hiyo utarahisisha mawasiliano kati ya Nyakato na maeneo mengine, ikiwemo njia ya kuelekea machimbo ya dhahabu, huku wanafunzi wa Shule ya Msingi Maila wakitarajiwa kunufaika kwa kuondokana na changamoto ya kushindwa kufika shuleni kipindi cha mvua.



Hussein amewashukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge Benjamin Ngayiwa, Meya Mataluma Kaniki na TARURA kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kufanikisha kuanza kwa mradi huo, akieleza kuwa utachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo la Nyakato na Manispaa ya Kahama kwa ujumla.


Post a Comment

Previous Post Next Post