" MITAMBO YA KISASA YA KUCHENJUA DHAHABU YAIBADILI SEGESE; YALETA AJIRA, WAWEKEZAJI WATAKA SERIKALI IIMARISHE UTAFITI WA MADINI

MITAMBO YA KISASA YA KUCHENJUA DHAHABU YAIBADILI SEGESE; YALETA AJIRA, WAWEKEZAJI WATAKA SERIKALI IIMARISHE UTAFITI WA MADINI

Na Paul Kayanda, KahamaKata ya Segese, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, imeanza kuandika historia mpya katika sekta ya madini baada ya kuanzishwa kwa mitambo miwili ya kisasa ya kuchenjua dhahabu yenye uwezo wa kuchakata jumla ya tani 300 za mchanga wa dhahabu kwa siku, hatua inayotajwa kuongeza thamani ya madini, kutoa ajira kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.Mitambo hiyo imejengwa na kampuni ya Ilelema Gold Plant, inayomilikiwa na mzawa wa Kijiji cha Segese, Leonard Makune, ikiwa ni miongoni mwa wawekezaji wazawa wanaoendelea kuwekeza katika kuongeza thamani ya madini yanayochimbwa nchini.Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea kiwanda hicho, Mhandisi wa Uchenjuaji wa Madini, Philibert Teyanga, alisema mradi huo ulianza rasmi mwezi Februari mwaka 2024 kwa kujengwa mtambo wa kwanza wenye uwezo wa kuchakata kati ya tani 80 hadi 100 za mchanga wa dhahabu kwa siku.Alisema mafanikio yaliyopatikana ndani ya mwaka mmoja wa uzalishaji yaliifanya kampuni kuongeza uwekezaji kwa kujenga mtambo mwingine mkubwa wenye uwezo wa kuchakata kati ya tani 180 hadi 200 kwa siku, hivyo kufanya uwezo wa kiwanda kufikia tani 300 kwa siku."Tulianza uzalishaji Februari mwaka 2024 kwa kutumia mtambo mdogo wenye uwezo wa kuchakata tani 80 hadi 100 kwa siku. Kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji na ushirikiano tunaoupata kutoka Serikalini, tumeweza kuongeza mtambo mkubwa unaochakata hadi tani 200 kwa siku," alisema Teyanga.Alisema uwekezaji huo unaonyesha jinsi Watanzania wanavyozidi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kwa kuwekeza katika teknolojia ya kisasa inayoongeza thamani ya rasilimali za nchi badala ya kuuza malighafi pekee.Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Ilelema Gold Plant, Baluhi Makoye Baluhi, alisema pamoja na mafanikio ya uzalishaji, kampuni imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wa eneo la Segese na vijiji vya jirani.Alieleza kuwa hadi sasa kampuni imeajiri wafanyakazi wa kudumu 14, huku kila mwezi ikitoa ajira za muda kwa watu kati ya 40 na 50, wengi wao wakiwa wakazi wa eneo hilo."Katika kipindi kifupi tangu tuanze uzalishaji, tumefanikiwa kuajiri wafanyakazi wa kudumu 14 na kutoa ajira za muda kwa watu hadi 50 kila mwezi. Lengo letu ni kuendelea kupanua uzalishaji ili kuongeza ajira na kuchangia maendeleo ya wananchi," alisema Baluhi.Mbali na kutoa ajira, alisema shughuli za kiwanda hicho zimechochea ukuaji wa biashara mbalimbali ikiwemo usafirishaji, huduma za chakula, makazi na biashara ndogondogo zinazowategemea wafanyakazi na shughuli za uzalishaji wa madini.Hata hivyo, alisema pamoja na mafanikio hayo, kampuni inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa malighafi zenye kiwango kikubwa cha dhahabu.Alifafanua kuwa mawe mengi yanayowasilishwa kiwandani na wachimbaji wadogo yanakuwa na kiwango kidogo cha madini kutokana na uchimbaji unaofanyika bila utafiti wa kitaalamu, jambo linaloongeza gharama za uzalishaji na kupunguza faida."Tunapata mawe yenye kiwango kidogo cha dhahabu kwa sababu wachimbaji wengi bado wanachimba kwa kubahatisha. Matokeo yake ni kwamba gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa kuliko mapatotunayopata," alieleza.Kutokana na changamoto hiyo, Meneja huyo aliiomba Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya muungano Wa Tanzania pamoja na wasaidizi wake akiwemo waziri wakili Anthony Mavunde ihakikishe inaendelea kuunga mkono wawekezaji wa ndani kwa kuwezesha upatikanaji wa mitambo ya kisasa ya kufanya utafiti wa kijiolojia katika maeneo yenye leseni za uchimbaji.Alisema matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utafiti yatawawezesha wachimbaji kubaini maeneo yenye madini mengi, kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uchimbaji na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa.Kwa mujibu wa viongozi wa kampuni hiyo, matarajio yao ni kuendelea kupanua uwekezaji, kuongeza uwezo wa uzalishaji na kutoa ajira zaidi kwa vijana, huku wakisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji na wachimbaji wadogo ndio msingi wa maendeleo endelevu ya sekta ya madini nchini.Uwekezaji wa Ilelema Gold Plant unatajwa kuwa mfano wa namna uwekezaji wa wazawa unavyoweza kuongeza thamani ya madini, kuibua fursa za ajira na kuleta maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ya uzalishaji wa madini, huku ukiifanya Segese kuendelea kujipambanua kama moja ya maeneo yanayokuwa kwa kasi katika sekta ya madini wilayani Kahama.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post