" NAIBU WAZIRI AIMWAGIA SIFA ATOZ, KWA KUWEKEZA BIL20 UJENZI KIWANDA CHA KUZALISHA DAWA NA VIFAA TIBA

NAIBU WAZIRI AIMWAGIA SIFA ATOZ, KWA KUWEKEZA BIL20 UJENZI KIWANDA CHA KUZALISHA DAWA NA VIFAA TIBA

Na Seif Mangwangi Arusha 

Serikali imeipongeza Kampuni ya A to Z Group kwa kuwekeza zaidi ya Sh20 bilioni katika ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kutengeneza dawa na vifaa tiba katika eneo la Kisongo, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha na kusema kuwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya afya, kukuza uchumi wa viwanda na kupunguza utegemezi wa bidhaa za tiba kutoka nje ya nchi.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Julai25, 2026 Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais , Mipango na Uwekezaji, Dk. Pius Chaya, amesema uwekezaji huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekeleza maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda na uwekezaji wa ndani. 

 Amesema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitumia fedha nyingi za kigeni kuagiza dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi, hali ambayo Serikali inalenga kuibadilisha kupitia kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hizo nchini ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya kwa wakati na kwa gharama nafuu, pamoja na kuimarisha usalama wa afya kwa wananchi.
Dkt. Chaya aliisifu Menejimenti ya kiwanda Cha A to Z Group kwa kuonyesha uzalendo kwa kuwekeza katika sekta nyeti ya afya, akisema mradi huo utazalisha ajira nyingi, kuhamisha teknolojia za kisasa na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa dawa na vifaa tiba katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

Pia amesema Serikali inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Tano wa Taifa wa Maendeleo, ambayo yanatoa kipaumbele katika kukuza viwanda vya ndani kupitia sera rafiki kwa wawekezaji. 

Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha AtoZ Kaplesh Shah amesema pamoja na uwekezaji huo, bado wanaokabiliwa na changamoto ya ubovu wa Barabara kuelekea kiwandani hapo, kutopatikana kwa umeme wa uhakika hali inayosababisha uzalishaji kupunguza.

Akijibu changamoto hizo, Naibu Waziri Dkt. Chaya amesema Serikali tayari imetenga rasilimali kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika maeneo muhimu ya uwekezaji ili kuhakikisha viwanda vinafanya kazi kwa ufanisi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika masoko ya kimataifa. 

Meneja wa Masoko na Ushirikiano wa Kimataifa wa A to Z Group, Silvester Kazi, amesema kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Sh20 bilioni katika kiwanda hicho ili kuongeza uwezo wa Tanzania kuzalisha vifaa tiba muhimu vinavyotumika kila siku katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya. 

Amesema kupitia kiwanda hicho kutazalishwa bidhaa mbalimbali zikiwemo sindano, vifaa vya kupitishia dawa kwa njia ya mshipa na vifaa vya kuongezea wagonjwa damu, ambavyo vina mahitaji makubwa nchini na katika masoko ya kikanda.
"Kiwanda hiki kina teknolojia ya kisasa inayozalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa vya ubora. Mbali na kuongeza ajira, kitaimarisha sekta ya afya na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa mzalishaji mkubwa wa vifaa tiba katika ukanda huu," amesema Kazi. 

Kazi amesema A to Z Group ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wazawa nchini, ikiwa na zaidi ya wafanyakazi 6,000, huku kiwanda kipya kikitarajiwa kuajiri mamia ya Watanzania wengine na kuchochea ukuaji wa sekta ya utengenezaji wa bidhaa za afya.

 Ziara ya Dk. Chaya katika kiwanda hicho imeonekana kama ishara ya dhamira ya Serikali ya kuendelea kuvutia uwekezaji wa kimkakati unaochochea uhamishaji wa teknolojia, kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa za tiba kutoka nje. 

 Mradi huo pia unatarajiwa kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa dawa na vifaa tiba katika masoko ya Afrika Mashariki na Kati.

Post a Comment

Previous Post Next Post