" SAMIA SCHOLARSHIP KUZALISHA WATAALAMU WA AI, DATA SCIENCE NA TEKNOLOJIA ZA KISASA

SAMIA SCHOLARSHIP KUZALISHA WATAALAMU WA AI, DATA SCIENCE NA TEKNOLOJIA ZA KISASA



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari jana Julai 27,2026 jijini Dodoma kuhusu uteuzi wa wanafunzi 1,050 waliofanya vizuri zaidi katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita 2026, kunufaika na ufadhili wa masomo kupitia programu ya Samia Scholarship.
Na.Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI imewateuwa wanafunzi 1,050 waliofanya vizuri zaidi katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita 2026, kunufaika na ufadhili wa masomo kupitia programu ya Samia Scholarship, huku wanafunzi 50 wakipata nafasi ya kusoma katika vyuo vikuu vinavyoongoza duniani kwa ufadhili wa asilimia 100.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 27,2026 jijini Dodoma ,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,amesema kati ya wanafunzi hao, 1,000 watasoma katika vyuo vikuu vya ndani, huku Serikali ikigharamia gharama zote za masomo yao.
Amesema wanafunzi 50 watakaosoma nje ya nchi watafadhiliwa kikamilifu, ikiwemo ada, gharama za maisha na mahitaji mengine muhimu, katika vyuo vinavyotambulika kimataifa kwa ubora katika fani za sayansi na teknolojia.
"Mpango huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu kwa kugharamia kwa asilimia 100 masomo ya wanafunzi bora, ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu katika sayansi na teknolojia," amesema Prof. Mkenda.
Amesema wanaostahili kunufaika na mpango huo ni wanafunzi watakaojiunga na shahada za kwanza katika fani za Hisabati, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Uhandisi na Tiba.
Prof. Mkenda amesema wanafunzi wote watakaopata udahili katika vyuo husika wanapaswa kujaza fomu za maombi ya Samia Scholarship ili Serikali ianze mchakato wa kugharamia masomo yao.
"Wanafunzi wote wanaostahili wanatakiwa kujaza fomu za maombi mara baada ya kupata udahili ili waweze kunufaika na mpango huu," amesema .
Kwa mujibu wa Prof. Mkenda, asilimia 58 ya wanafunzi waliochaguliwa wanatoka katika shule za Serikali, huku asilimia 42 wakitoka shule binafsi.
Amesema wanafunzi 50 waliopata ufaulu wa juu zaidi katika tahasusi za PCM, PGM na PMC, wakiwa na alama tatu za daraja A, wamechaguliwa kwenda kusoma katika vyuo vya nje ya nchi katika fani za teknolojia za kisasa, zikiwemo Akili Unde (Artificial Intelligence) na Sayansi ya Data (Data Science).
Aidha, amesema wanafunzi watakaokubali ufadhili huo watatakiwa kujaza fomu za uthibitisho kabla ya kushiriki mafunzo maalumu ya maandalizi (Bootcamp) yatakayofanyika katika Chuo cha Nelson Mandela, Arusha, kabla ya kuanza safari ya masomo yao nje ya nchi.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha programu hiyo kama sehemu ya jitihada za kuandaa wataalamu watakaosaidia kuharakisha maendeleo ya taifa kupitia sayansi, teknolojia na ubunifu.

Post a Comment

Previous Post Next Post