
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb),
ametoa maagizo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mkandarasi na wadau
wote wanaotekeleza awamu ya pili ya mradi wa Umeme wa Jua uliopo Wilaya ya
Kishapu Mkoani Shinyanga kuhakikisha mradi huo unasimamiwa kwa ukaribu na
kukamilika ndani ya muda wa miezi 17 uliopangwa, ili kuendelea kuimarisha
upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Maagizo hayo ameyatoa leo Julai 27, 2026, mara baada
ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 204.7
kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni za Sagemcom Energy &
Telecom SAS pamoja na STEG International Services kwa ajili ya utekelezaji wa
Awamu ya Pili ya Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa kuzalisha
Megawati 100 katika eneo la Ngunga, Wilaya ya Kishapu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ndejembi amesema
TANESCO ina wajibu wa kuhakikisha kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo
inafuatiliwa kwa karibu ili kazi ifanyike kwa ubora unaotakiwa na kukamilika
kwa wakati, akisisitiza kuwa mradi huo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa
umeme nchini kupitia vyanzo vya nishati jadidifu.
Aidha, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo
kuzingatia kikamilifu masharti yote ya mkataba, ikiwemo ratiba ya utekelezaji
wa kazi, viwango vya ubora wa ujenzi, usalama mahali pa kazi pamoja na ulinzi
wa mazingira, akieleza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaoathiri
utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Vilevile, Waziri huyo ameitaka TANESCO kuendelea kutoa
elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi ili washiriki kikamilifu katika
kuulinda, akisema ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha
miundombinu ya maendeleo inalindwa dhidi ya vitendo vya uharibifu.
Katika kuhakikisha manufaa ya mradi yanawanufaisha
wananchi wa eneo husika, Waziri Ndejembi pia amesisitiza kuwa mkandarasi
ahakikishe stahiki zote za wafanyakazi wazawa zinazingatiwa kwa mujibu wa
sheria, huku TANESCO ikiendelea kutoa kipaumbele kwa wahandisi na wataalamu
wazawa kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Mbali na hilo, Waziri huyo ameitaka TANESCO kuongeza
mchango wake katika maendeleo ya jamii kupitia programu za Uwajibikaji kwa
Jamii (CSR), kwa kujenga madarasa matano mapya katika eneo la mradi, tofauti na
madarasa matatu yaliyojengwa wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza.
Akizungumzia mradi huo, Waziri Ndejembi amesema
Serikali imeendelea kuwekeza katika mseto wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme
(Energy Mix), ambapo Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu ni sehemu ya mkakati wa
kuongeza uzalishaji wa umeme wa gharama nafuu na unaotokana na nishati
jadidifu.
Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili
zenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 150. Awamu ya kwanza yenye uwezo wa
Megawati 50 iligharimu Shilingi bilioni 118.3 na kwa sasa ipo katika hatua za
mwisho za utekelezaji, huku awamu ya pili yenye uwezo wa Megawati 100
ikigharimu Shilingi bilioni 204.7, hivyo kufanya gharama za jumla za mradi
kufikia Shilingi bilioni 323.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kukamilika kwa mradi huo
kutachangia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vya nishati jadidifu,
kuimarisha uthabiti wa mfumo wa umeme nchini na kusaidia Serikali kufikia lengo
la kuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya sasa na ya baadaye.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome
Makamba, amesema Wizara ya Nishati na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga
watausimamia mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ubora na
kukamilika kama ilivyopangwa.
Amesema mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa
awamu ya kwanza yanatoa matumaini kuwa awamu ya pili pia itatekelezwa kwa
ufanisi mkubwa, huku akisisitiza kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa
wananchi wa Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, ameahidi
kuwa shirika hilo litamsimamia mkandarasi kwa karibu katika kila hatua ya
utekelezaji ili kuhakikisha kazi zote zinafanyika kwa ubora unaotakiwa na mradi
unakamilika ndani ya muda uliokubaliwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi, Joao Jirio,
amesema kampuni hiyo ipo tayari kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia masharti
yote ya mkataba na kuhakikisha unakamilika kwa wakati, huku ukifikia viwango
vya kimataifa vya ubora.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia
Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, pamoja na viongozi
mbalimbali wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi na wadau wa sekta ya nishati.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






























Post a Comment