NA: MWANDISHI WETU, DODOMA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (MCC), Mary Chatanda, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda Tume ya Kuchunguza Wahusika wa Ghasia za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Chatanda ametoa pongezi hizo, Agosti 09, 2026, Jijini Dodoma. Amesema, Rais Dk. Samia ameonyesha dhamira ya kujenga upya taifa lenye umoja na mshikamano, ndiyo maana ameunda Tume hiyo.
"Kipekee nimpongeze Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuunda Tume yenye wataalamu na wabobezi wa masuala mbalimbali ya kisheria wa ndani na nje ya nchi, naamini kwa Hadidu za Rejea walizonazo, watakuja na majibu ya maswali mengi waliyonayo wananchi," amesema Chatanda.
Vilevile, amesema, ni vyema wananchi wakaiacha Tume hiyo ifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria badala ya kuikosoa kabla ya kutekeleza kazi yake.
"Ipo kasumba mbaya kwa baadhi ya watu kukosoa Tume inapoundwa hata kabla haijaanza utekelezaji wa majukumu yake, ni vyema tuiache Tume iwe huru ifanye kazi yake," ameongeza.
AWAKOSOA WANAOSEMA TUSITAFUTE MCHAWI WA VURUGU
Mwenyekiti huyo wa UWT Taifa, amekosoa baadhi ya watu wanaosema Tume ya Kuchunguza Wahusika wa Ghasia ijikite katika kujenga maridhiano kuliko kutafuta mchawi wa vurugu za Uchaguzi.
"Wale wanaosema Tume isitafute mchawi, wanakosea sana, niseme tu ya kwamba mchawi lazima afahamike, hatuwezi kujenga maridhiano katika mazingira ambayo hatuna majibu ya kiutafiti, kitaalamu na kisayansi ya nani ni wahusika halisi wa vurugu zile," amesisitiza.
Ikumbukwe kuwa, Agosti 07, 2026, Rais Dk. Samia alizindua Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jijini Dar es Salaam.
Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila, huku ikipewa miezi mitano yaani siku 150 za uchunguzi, kukamilisha kazi, kuwasilisha taarifa na mapendekezo yake.
Katika uzinduzi huo, Rais Samia alisema "Niwasihi sana Watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika na Tume katika kutekeleza majukumu yao. Tusaidie Tume hii iweze kufanya kazi yake na tusiisumbue".
Tume hiyo ina wajumbe sita akiwemo Mwenyekiti wake, wanne wakiwa ni Watanzania huku wawili wakitokea katika nchi za Namibia na Uganda.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment