" ELIMU YA VIPIMO YAWASAIDIA WAJASIRIAMALI NANE NANE KUBORESHA BIDHAA NA KUPANUA SOKO

ELIMU YA VIPIMO YAWASAIDIA WAJASIRIAMALI NANE NANE KUBORESHA BIDHAA NA KUPANUA SOKO

Na. WMA- DODOMA

Wakala wa Vipimo (WMA) imetoa elimu kwa wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Nane Nane Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela Nzuguni  jijini Dodoma, kuhusu umuhimu wa ufungashaji na uwekaji wa taarifa sahihi kwenye bidhaa ili kuongeza ushindani katika soko.

Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo Agosti 2, 2026, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Singida, Willie Amos, amesema kuwa wamefika katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa ajili ya kukagua bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali pamoja na kutoa maelekezo ya namna ya kuziboresha.

Amesema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kuangalia namna bidhaa zilivyofungashwa na kuwashauri wajasiriamali kuhusu maboresho yanayoweza kufanyika ili bidhaa zao ziweze kupata soko ndani na nje ya nchi.

“Katika ukaguzi ambao tumeufanya hapa leo, tumebaini wajasiriamali wanazalisha bidhaa ambazo ni nzuri lakini zina baadhi ya mapungufu ambayo wakiyaboresha yataongeza soko na tija kwenye shughuli zao za uzalishaji,” amesema Amos.

Amebainisha kuwa baadhi ya bidhaa za asili walizoziona kama dengu zina muonekano mzuri lakini hazina taarifa muhimu zinazohitajika kwenye bidhaa, hivyo amewashauri wajasiriamali kuboresha eneo hilo ili kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Aidha, amesema kuwa wameona bidhaa za sabuni zinazozalishwa na wajasiriamali hao ambazo zimeweka taarifa za mzalishaji, lakini bado kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kuboreshwa ili ziweze kufikia viwango vinavyohitajika sokoni.

Pia ameongeza kuwa baadhi ya bidhaa nyingine hazina taarifa kabisa licha ya kuwa na ubora na mahitaji katika soko, akitolea mfano mahindi yaliyochemshwa ambayo hayajaoneshwa taarifa muhimu kama jina la bidhaa na kiwango kilichopo kwenye kifungashio.

Kwa upande wake, Husseini Maghembe Husseini kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, amesema kuwa wanashiriki Maonesho ya Nane Nane wakiwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta ya alizeti, karanga, dengu, pamba pamoja na mahindi yaliyochemshwa na kukaushwa.

Amesema kuwa kupitia elimu waliyoipata kutoka Wakala wa Vipimo wameweza kutambua umuhimu wa kuweka nembo (logo), mawasiliano ya mzalishaji na taarifa nyingine muhimu kwenye bidhaa zao ili kurahisisha upatikanaji wa wateja.

“Bidhaa zetu zilikuwa zinakuja bila logo, kwa hiyo uuzaji wetu ulikuwa unakuwa tabu pale mtu anapotaka kututafuta tunapatikana kwa njia gani. Tumepata elimu namna ya kupima na kubrand bidhaa zetu,” amesema Husseini.

Ameongeza kuwa elimu hiyo imewasaidia na kuahidi kuwa katika maonesho yajayo watawasilisha bidhaa zilizokamilika zikiwa na taarifa zote muhimu pamoja na mawasiliano yao.

Naye Jackline Lishaberi, Msimamizi wa Manzuki kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) upande wa Manyoni, amesema wamepata msaada mkubwa kutoka Wakala wa Vipimo katika kuboresha bidhaa zao hasa kwenye eneo la uhifadhi wa asali na matumizi sahihi ya lebo.

Amesema kuwa wameelekezwa namna ya kuweka lebo kwa usahihi kulingana na ukubwa wa vifungashio pamoja na upangaji wa maandishi ili bidhaa zao ziweze kuvutia zaidi katika soko.

Amebainisha kuwa awali walikuwa na changamoto kwenye uwekaji wa lebo hasa kwenye bidhaa za nta na bidhaa nyingine walizokuwa wakiziweka kama maonesho, lakini baada ya kupata elimu wameweza kufahamu namna bora ya kuboresha.

“Watu wa vipimo wametuelekeza namna nzuri ya kuweka label kwa uwiano ulio sawa ili kuweza kuelimisha watu zaidi lakini kuvutia ile biashara, ile bidhaa iweze kwenda katika mfumo mzuri wa kibiashara,” amesema Jackline.

Post a Comment

Previous Post Next Post