Yawataka wananchi kujiunga mapema kujikinga na gharama za matibabu
Na Grace Michael, Dodoma
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewahimiza wananchi nchini kujiunga na bima ya afya kabla ya kuugua, ukieleza kuwa ni njia salama ya kujikinga dhidi ya gharama kubwa za matibabu ambazo zinaweza kujitokeza wakati wowote.
Wito huo umetolewa leo Agosti 07, 2026 na Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja wa NHIF, Angela Mziray, wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la Mfuko katika Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, mkoani Dodoma.
Bi. Mziray amesema maonesho hayo yameipa NHIF fursa ya kuwafikia wananchi wengi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za matibabu bila vikwazo vya kifedha.
Amesema changamoto za kiafya zinaweza kumpata mtu yeyote bila kutarajia, na mara nyingi husababisha familia nyingi kutumia akiba zao au hata kuuza mali ili kugharamia matibabu.
“Ugonjwa huja bila taarifa. Unaweza kuwa mzima leo lakini kesho ukahitaji matibabu ya gharama kubwa. Ndiyo maana tunawahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya mapema ili wajenge kinga ya kifedha kwao na kwa familia zao," amesema Bi. Mziray.
Amefafanua kuwa mwananchi anapochangia bima ya afya kabla hajaugua, hupata uhakika wa matibabu bila kubeba mzigo mkubwa wa gharama wakati wa uhitaji.
“Ni muhimu wananchi wajidundulize kidogo kidogo na kuchangia bima ya afya. Hii ndiyo njia bora ya kuhakikisha familia inapata huduma za matibabu kwa wakati bila kuathiri mipango ya maendeleo," amesema.
Bi. Mziray amesema NHIF inaendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za bima ya afya na kuhamasisha matumizi ya mfumo wa bima badala ya kulipia matibabu moja kwa moja kutoka mfukoni.
Ameongeza kuwa wanachama wa NHIF wanapata huduma katika mtandao mpana wa vituo vya afya vya Serikali, binafsi na vya mashirika ya dini vilivyosajiliwa na Mfuko, jambo linalowapa urahisi wa kupata huduma popote wanapozihitaji.
Aidha, amesema kuwa na bima ya afya siyo tu kulinda afya ya mtu binafsi, bali pia ni kulinda uchumi wa familia kwa kupunguza matumizi yasiyotarajiwa yanayotokana na matibabu.
Katika Maonesho ya Nanenane, NHIF inaendelea kutoa huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa wanachama wapya, elimu kuhusu vifurushi vya bima ya afya, ushauri kwa wanachama pamoja na ufafanuzi wa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.
Wananchi wanaotembelea banda la NHIF pia wanapata fursa ya kuuliza maswali, kupata majibu kuhusu huduma za Mfuko na kujiunga na bima ya afya papo hapo, hatua inayochangia kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na kinga ya kifedha dhidi ya gharama za matibabu.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment