

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wadau wa sekta ya kilimo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), huku mtaji wa benki hiyo ukiongezeka kutoka Sh bilioni 60 mwaka 2020/21 hadi Sh bilioni 452.
Rais Samia amesema hayo leo, Agosti 8, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya kufunga Maonesho ya Nanenane 2026 yaliyofanyika mkoani Dodoma, ambapo alikuwa Mgeni Rasmi.
Amesema ongezeko hilo la mtaji limeongeza uwezo wa TADB kutoa mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, hatua inayolenga kuchochea uzalishaji na kukuza uchumi kupitia sekta ya kilimo.
Aidha, Rais Samia ameipongeza TADB na kuipatia tuzo kwa kuwa Mdhamini Mkuu wa Maonesho ya Nanenane 2026, akisema ushiriki wa benki hiyo umeendelea kuonesha dhamira ya Serikali na taasisi zake katika kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kuwaunganisha wananchi na fursa za mitaji, teknolojia na uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imefungua milango ya fursa za kiuchumi kwa zaidi ya Watanzania milioni 2.6 kupitia mikopo na uwekezaji, hatua inayochangia kubadili kilimo kutoka uzalishaji wa kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara chenye tija na ushindani.
Amesema TADB imetoa mikopo yenye thamani ya Sh trilioni 1.55 kwa miradi 862, ambapo Sh trilioni 1.32, sawa na asilimia 84, zimetolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Nyabundege amesema fedha hizo zimeelekezwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ikiwemo ujenzi wa mifumo ya umwagiliaji, maghala, vihenge na viwanda vya uchakataji, kwa lengo la kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko.
Amesema Sh bilioni 611.8 zimeelekezwa katika mazao ya chakula, huku Sh bilioni 884.24 zikiwekezwa katika sekta za kimkakati zikiwemo mafuta ya kula, kahawa, korosho, sukari na pamba.
Aidha, amesema kupitia Mfuko wa Dhamana wenye mtaji wa Sh bilioni 108, TADB imewezesha mikopo ya Sh bilioni 692 kwa wakulima wadogo kupitia taasisi 21 za kifedha, na kuwafikia zaidi ya wanufaika 657,000.
Nyabundege amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na ongezeko la mtaji wa benki kutoka Sh bilioni 60 hadi Sh bilioni 452, ambapo Sh bilioni 392, sawa na asilimia 86.7, zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema mafanikio ya TADB hayapimwi kwa tuzo pekee, bali kwa matokeo yanayowagusa wananchi, ikiwemo kuongezeka kwa usalama wa chakula, ajira, masoko na kipato cha familia.
Amesema TADB itaendelea kutumia mikopo na dhamana za mikopo kuchochea mageuzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara kinachotumia teknolojia na kuongeza thamani ya mazao.
TADB ilikuwa Mdhamini Mkuu wa Maonesho ya Nanenane 2026, yaliyolenga kuonesha fursa za uwekezaji, ubunifu na teknolojia katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.







SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment