" RC asema utamaduni ni nguzo ya maadili, mshikamano

RC asema utamaduni ni nguzo ya maadili, mshikamano


MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema kuwa utamaduni ni nguzo kuu ya kulinda maadili ya Mtanzania, kujenga mshikamano na kuimarisha uzalendo wa kitaifa.

Malima alisema hayo akifungua Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni mwaka 2026 linalofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Akizungumza katika hafla hiyo, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika mabanda mbalimbali ili kujifunza mila, desturi, vyakula vya asili na dawa za kienyeji kutoka mikoa yote nchini.

Pia, alieleza kuwa matumizi sahihi ya utamaduni na urithi yanapaswa kuwa fursa ya kujitangaza na kujiandaa vizuri kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Malima aliwasili katika viwanja hivyo na kutembelea mabanda ya mikoa mbalimbali inayoshiriki tamasha hilo na kutazama maonesho ya vyakula, dawa za asili, mavazi pamoja na mila na desturi zinazopatikana katika mikoa husika.

Tamasha hilo linakutanisha wadau wa utamaduni kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuonesha, kutunza na kukuza urithi wa Kitanzania. Zaidi ya wananchi 150,000 kutoka mikoa yote nchini wanashiriki, huku kukiwa na vikundi 25 vya ngoma za asili na wasanii zaidi ya 30.

Post a Comment

Previous Post Next Post