" SAMIA, AFDB WAAHIDI USHIRIKIANO MPYA KUHARAKISHA MAGEUZI KIUCHUMI

SAMIA, AFDB WAAHIDI USHIRIKIANO MPYA KUHARAKISHA MAGEUZI KIUCHUMI




Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Sidi Ould Tah, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano thabiti katika kufadhili miradi ya kimkakati ili kuharakisha mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania na kuwezesha utekelezaji wenye mafanikio wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo rasmi yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadili kwa kina uwekezaji katika sekta za nishati, usafiri, mtangamano wa kikanda na mifumo bunifu ya kupata fedha za maendeleo, huku Rais Samia akiishukuru benki hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kufadhili miradi mikubwa kama vile Reli ya Kisasa (SGR), miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART), barabara za kimkakati, na usambazaji wa umeme.

Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zimetilia mkazo utekelezaji wa mpango wa kimataifa wa Mission 300 unaolenga kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030, ambapo Dk. Tah ameongeza kuwa AfDB inaendelea na mageuzi ya ndani ili kupunguza muda wa kuidhinisha miradi na kuvutia uwekezaji zaidi kutoka sekta binafsi, akiahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kufanikisha maendeleo endelevu na upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi wote.

Post a Comment

Previous Post Next Post