Kampuni ya uchapishaji wa vitabu vya shule Tanzania Bara na Zanzibar, Semuka International Ltd, imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuunga mkono sekta ya elimu nchini kwa kuchangia vitabu na madaftari kwa Mwanamke Initiatives Foundation, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza elimu bora kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Mchango huo umetolewa wakati wa Tamasha la Kizimkazi Festival, ambapo Mkurugenzi wa Masoko wa Semuka International Ltd, Walii Hassan Miyonga, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Erick R. Katabaro, amesema kuwa lengo kuu la Semuka International Ltd ni kushiriki kikamilifu katika kuboresha elimu nchini kwa kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi mashuleni.
Amesema kampuni hiyo inaamini kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunzia kupitia upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kujifunzia.
Mchango huo umepokelewa na Mwenyekiti wa Mwanamke Initiatives Foundation, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Wanu Khafidh Ameir, mbele ya Mgeni Rasmi Mhe. Kwagilwa Ruben, Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mhe. Wanu Khafidh Ameir ameishukuru Semuka International Ltd kwa moyo wake wa kujitolea na kusaidia maendeleo ya elimu, akieleza kuwa mchango huo utasaidia kuongeza hamasa ya wanafunzi katika kujifunza na kufikia malengo yao ya kitaaluma.
Semuka International Ltd ni kampuni inayojihusisha na uchapishaji wa vitabu vya shule, usambazaji wa vifaa vya TEHAMA (ICT Equipment) kwa taasisi na ofisi mbalimbali, usambazaji wa samani za ofisini pamoja na umiliki wa kampuni za usafirishaji, ikiwa ni miongoni mwa kampuni zinazochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment