" SERIKALI YATOA ONYO DHIDI YA UDHALILISHAJI MTANDAONI

SERIKALI YATOA ONYO DHIDI YA UDHALILISHAJI MTANDAONI




Serikali imeitaka jamii kutokubali vitendo vya udhalilishaji mitandaoni vionekane kuwa jambo la kawaida, huku ikionya kuwa tabia hiyo inaweza kuharibu mustakabali mzima wa taifa.


Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima, katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.


Katika mazungumzo hayo, Dkt. Gwajima alisisitiza kuwa madhara ya unyanyasaji wa mtandaoni hayabaki kwa mtu mmoja pekee anayelengwa, bali huenea na kuathiri familia nzima, watoto, na mahusiano ya kijamii, hali inayoweza kuzaa utamaduni mbaya unaorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa mapema.


Akielezea hofu yake juu ya mwelekeo wa kizazi kipya, Waziri huyo alihoji aina ya maadili yatakayojengwa kwa siku za usoni ikiwa jamii itaendelea kushangilia unyanyasaji wa mtandaoni, ikizingatiwa kuwa vijana wa leo ndio wazazi na viongozi wa kesho.

Alifafanua kuwa kukemea vitendo hivyo si chuki dhidi ya vijana, bali ni jitihada za kuwaokoa na kuwakumbusha wajibu wao wa kuheshimu utu, staha, na sheria za nchi ambazo wengi hupuuzwa wakidhani kuwa ulimwengu wa mtandao hauna sheria.

Alionya kuwa baadhi ya wanaofanya vitendo vya kuwatukana au kuwanyanyasa wenzao mitandaoni huenda wasitambue uzito wa sheria mpaka pale watakapokabiliwa na mikono ya sheria kutokana na malalamiko ya waathirika.

Kuhusiana na suala la upatikanaji wa haki, Dk Gwajima alitoa wito maalum kwa wanasheria kutumia taaluma yao kusaidia wananchi wanaoathirika na unyanyasaji huo, hasa ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya watu wenye uwezo wa kifedha wanaotaka kutumia nafasi zao kuwakandamiza wengine.

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano mpana kati ya serikali, taasisi mbalimbali, viongozi wa dini, na wazazi katika kutoa elimu endelevu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, akihimiza kuwa uhuru wa kutumia mitandao lazima uende sambamba na uwajibikaji, heshima, na utii wa sheria.

Post a Comment

Previous Post Next Post