
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha Zawadi Ngailo akizungumza katika warsha hiyo jijini Arusha leo

Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla akizungumza katika warsha hiyo jijini Arusha leo

……..
Na Happy Lazaro, Arusha.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imewakutanisha wadau wa usimamizi na utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo mkoa wa Arusha ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji, uadilifu na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Warsha hiyo imelenga kujenga mtazamo wa pamoja, kubaini changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi na kuweka mikakati ya kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza katika warsha hiyo,Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema kuwa TAKUKURU ina jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa kwa mujibu wa sheria, kupitia uzuiaji, uchunguzi na utekelezaji wa sheria, huku ikishirikiana na taasisi mbalimbali katika kuimarisha mifumo ya utendaji na utoaji wa huduma.
Amesema kuimarisha mifumo hiyo husaidia kubaini mianya ya rushwa na kutoa ushauri wa namna ya kuiziba, huku ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma, maarufu kama “Public Expenditure Tracking Survey” (PETS), ukiwa miongoni mwa mbinu zinazotumika katika kufuatilia utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo.
Ngailo amesema kuwa, katika ufuatiliaji huo, TAKUKURU imefanya uchunguzi na ufuatiliaji wa programu na miradi ya maendeleo 164 yenye thamani ya Shilingi bilioni 469 ambapo miradi 109 ilibainika kuwa na kasoro au dosari zilizohitaji maboresho.
“Kutokana na hali hiyo, TAKUKURU ilitoa mapendekezo 452 kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha miradi hiyo, huku mapendekezo hayo yakifikishwa kupitia vikao, warsha na barua. “amesema Ngailo.
Amesema changamoto zilizobainika ni pamoja na matumizi yasiyofaa ya rasilimali, ufuatiliaji usioridhisha, ucheleweshaji wa baadhi ya miradi na ushiriki mdogo wa wadau katika usimamizi na ufuatiliaji.
Ngailo ameongeza kuwa, changamoto hizo zinaweza kusababisha miradi kutekelezwa nje ya muda, kutofikia malengo yaliyokusudiwa au kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wananchi, hivyo warsha hiyo ni muhimu katika kutafuta suluhisho la pamoja.
Amefafanua kuwa,mikakati itakayowekwa inalenga kuhakikisha programu na miradi ya maendeleo inatekelezwa bila upotevu wa rasilimali, kupunguza ucheleweshaji, kuongeza ushiriki wa wadau na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Aidha, amesema lengo kubwa ni kuhakikisha kunapatikana thamani ya fedha zinazotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika kikao hicho,Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla amesema kuwa,mapambano dhidi ya rushwa hayapaswi kuonekana kama kikwazo cha utekelezaji wa miradi, bali ni sehemu ya kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa na miradi inatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema viongozi wa halmashauri, taasisi za Serikali na TAKUKURU wanategemeana katika kutekeleza majukumu yao, hivyo ni muhimu kukaa pamoja, kukumbushana wajibu, kuimarisha uadilifu na kuondoa tofauti pamoja na mitazamo hasi.
“wakati mwingine baadhi ya watu hutumia kauli kwamba “TAKUKURU wanafuatilia” kama sababu ya kuchelewesha utekelezaji wa miradi, jambo ambalo linaweza kujenga chuki na taswira isiyofaa dhidi ya taasisi hiyo.”amesema CPA Makalla.
Amesisitiza kuwa TAKUKURU inapaswa kuendelea na kazi yake ya kufuatilia miradi, huku watendaji wa Serikali wakitambua kuwa ufuatiliaji huo unalenga kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa usahihi.
Amesema katika maeneo ambayo ufuatiliaji umefanyika, TAKUKURU imekuwa ikitoa taarifa zinazosaidia viongozi kupata hali halisi ya miradi na kuchukua hatua stahiki.
Pia amewataka watumishi, hususan wanaohusika na ukaguzi, kuwa makini na zawadi, huduma au “offer” wanazopewa wakati wa kutekeleza majukumu yao, na kusema kupokea huduma au zawadi kutoka kwa mtu anayekaguliwa kunaweza kuathiri uhuru na uadilifu wa mkaguzi kwani inaathiri maamuzi yake.
Amesema kuwa, Serikali hutenga mabilioni ya fedha kupitia bajeti kwa ajili ya maendeleo, hivyo iwapo fedha hizo zitatumika kwa uadilifu bila rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali, nchi inaweza kupata maendeleo makubwa zaidi.
“umuhimu wa TAKUKURU unaonekana katika nafasi yake ya kuchunguza na kufuatilia miradi mbalimbali, akisisitiza pia umuhimu wa ushirikiano na taasisi nyingine, ikiwemo Mahakama, viongozi wa dini, Jeshi la Polisi, wabunge na taasisi za Serikali. “amesema Makalla.
Amesema kuwa,taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinapowasilishwa kwa Rais, ni muhimu pia kuzingatia kazi za ufuatiliaji na uchunguzi zinazofanywa na TAKUKURU ili kupata picha pana ya matumizi ya rasilimali na utekelezaji wa miradi.
CPA Makalla amewataka TAKUKURU, taasisi zote za Serikali na watendaji kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa kila upande unategemeana katika kufikia lengo la kuongeza mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha uadilifu na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Amewasihi wadau wote kutekeleza wajibu wao kwa dhati na kwa wakati, akisisitiza kuwa kuzuia rushwa ni jukumu la kila mmoja. “Kuzuia rushwa ni jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu,” amesema, akieleza kuwa warsha hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano, kuondoa mapungufu na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo yaliyokusudiwa
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment