" UTEUZI WA NDEJEMBI UTHIBITISHO KUWA VIJANA WANAWEZA

UTEUZI WA NDEJEMBI UTHIBITISHO KUWA VIJANA WANAWEZA



WACHAMBUZI wa siasa wamesema uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitisha jina la Deogratius Ndejembi (43) kuwa Makamu wa Rais ni uthibitisho vijana wanaweza kushika nafasi za juu katika uongozi wa nchi.

Pia, wamesema kupendekezwa kwake ni fundisho kwa viongozi kuwa na utii wa mamlaka zilizowapa nafasi ya kuwatumikia wananchi.

Mchambuzi wa siasa, Hamiduni Marcel amesema mabadiliko hayo yanaonesha viongozi wanapaswa kuwa wavumilivu, wastahimilivu, wawe na nidhamu na waheshimu mamlaka.

“Viongozi wanatakiwa kuzingatia nidhamu, weledi na kutambua nafasi zao kwa umma. Pia, kuwa na ustahimilivu na uvumilivu sio jambo la kesho, unatakiwa kulifanya leo,” alisema Marcel.

Mjumbe wa Baraza Kuu Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Mapury alisema uteuzi wa Ndejembi unaonesha uongozi ni dhamana anayopewa mtu na anapaswa kuitumikia kwa weledi na utiifu mkubwa.

“Uongozi ni dhamana na kama ni dhamana, unaonesha Ndejembi anaingia kwenye rekodi ya kiongozi mdogo, vijana wadogo kabisa kwenye taifa wanaoaminiwa kuingia kwenye nafasi kubwa kwenye taifa akiwa na miaka 43,” alisema Mapury.

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Samwel Marwa alisema kupendekezwa kwa Ndejembi kunaonesha Rais Dk Samia Suluhu Hassan anataka mtu atakayemsaidia kwenye masuala ya diplomasia ya kimataifa.

“Huyu ni msaidizi wa rais, mshauri wake kwa umri wake bado ana nguvu ya kuzunguka ndani na nje ya nchi na popote atakapotumwa na ni mtu ambaye ndani ya CCM hana makundi kutokana na ugeni wa nafasi kubwa kubwa,” alieleza Marwa.

Aliongeza: “Rais ameangalia mtu ambaye hana makundi na hataleta mgawanyiko ndani ya chama na atawaleta wananchi wote katika nafasi yake kama makamu wa rais. Kuna utofauti mkubwa wa umri kati yake na rais tunaona kuwa rais alikuwa anatafuta mtu atakayekuwa mtiifu na kuwavuta vijana.”

Mchambuzi wa siasa, Soba Sanganya alisema uteuzi wa Ndejembi umesheheni utashi wa mamlaka ya uteuzi na amebeba sifa za kutengeneza daraja la utekelezaji wa vitu vinavyotarajiwa na wananchi.

Alisema Ndejembi anabeba sifa za kijana, ana nguvu na hivyo ana mvuto kwa vijana wengi, msikivu mwaminifu, mtiifu na sio mjivuni. Pia, hana makundi na habagui watu, sifa zilizomvutia rais kumpendekeza kuwa msaidizi wake.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Dk Doto Bulendu alisema Ndejembi atasaidia kuleta umoja, maridhiano na utendaji kazi mpya katika serikali ya Tanzania.

“Natarajia atakuwa kiungo kikubwa kati ya mamlaka na wananchi, atasaidia kusukuma kete kumshauri rais juu ya dhana dhima ya maridhiano,” alieleza Dk Bulendu.

“Ana rekodi nzuri ya kiutendaji, kitu ambacho kimeaminisha vyombo vya uteuzi kuwa huyu atakuwa mtu sahihi katika kumsadia rais.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Elisha Magolango alisema Ndejembi ni kiongozi mwadilifu, mchapakazi na hana makundi ndani ya serikali na CCM.

Post a Comment

Previous Post Next Post