Na. Jesca Kipingu, KIZOTA
Wataalamu wa afya kutoka Kituo cha Afya Kizota wamefika katika Shule ya Msingi Kizota, Kata ya Kizota, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwa ajili ya kutoa chanjo ya Polio kwa watoto wenye umri wa kuanzia miezi 0 hadi miaka 10, ikiwa ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa huo na madhara yake, ikiwemo ulemavu wa kudumu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Katibu wa Afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambaye pia ni Msimamizi wa Kampeni ya Chanjo ya Polio, Hapiness Kaungya, aliwashukuru wazazi kwa mwitikio mkubwa walioonesha katika kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo. Alisisitiza kuwa ushiriki wa wazazi na walezi ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya ugonjwa wa Polio.
Aidha, Kaungya aliitaka jamii kuendelea kupata na kuzingatia taarifa sahihi zinazotolewa na wataalamu wa afya ili kuondokana na dhana potofu kuhusu chanjo. Alisema kuwa ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla una mchango mkubwa katika kufanikisha kampeni hiyo na kulinda afya na ustawi wa watoto.
Kwa upande wake, Afisa Muuguzi Msaidizi II, Naomi Simon alisema kuwa zoezi la utoaji wa chanjo katika Shule ya Msingi Kizota limekuwa na mwitikio mzuri, jambo linaloonesha utayari wa wazazi na walezi kushirikiana na wataalamu wa afya. Aliwaomba wazazi kuendelea kutoa ushirikiano pale wataalamu wa afya watakapofika katika maeneo ya makazi yao kuwapatia watoto chanjo.
Nae Kiongozi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) wa Kata ya Kizota, Kabla Pima aliwapongeza wazazi wa kata hiyo kwa mwitikio chanya walioonesha, akieleza kuwa ushirikiano wao umechangia kurahisisha utekelezaji wa kampeni ya chanjo. Aliwasihi wazazi ambao watoto wao bado hawajapatiwa chanjo kuhakikisha wanawapeleka kupata huduma hiyo kwa manufaa ya afya na ustawi wao.
Kwa upande wake Mwalimu wa Afya wa Shule ya Msingi Kizota, Mwl. Adelmas Mmbando alisema kuwa amefurahi kushiriki katika zoezi hilo na kuwahimiza wazazi kuondokana na dhana potofu kuhusu chanjo.
Nae mwanafunzi wa Darasa la Nne, Martha Musa, alisema kuwa wazazi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha watoto wanakuwa na afya njema na kufikia ndoto zao kwa kuwapatia kinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kuathiri maisha yao.
Kwa ujumla, zoezi hilo linaendelea kuonesha umuhimu na ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, shule, wazazi na jamii katika kuhakikisha kila mtoto mwenye umri kuanzia mwezi 0-miaka 10 anapatiwa chanjo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254





Post a Comment