Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema amani na utulivu wa Zanzibar ni msingi mkuu wa uchumi wa visiwa hivyo, akisisitiza kuwa rasilimali hiyo ya amani ndiyo biashara yenyewe na maisha halisi ya wananchi.
Othman aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Pamoja ya Kufanyia Kazi Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa uliofanyika Ikulu mjini Unguja, akibainisha kuwa Zanzibar inategemea zaidi uchumi wa huduma ambao unahitaji mazingira tulivu ili kushamiri.
Alieleza kuwa wawekezaji wa ndani na nje hawawezi kupeleka mitaji yao katika eneo lisilo na utulivu, jambo ambalo linafanya ujenzi wa amani ya kudumu kuwa nguzo ya kupata uwekezaji wa maana na kuchochea ustawi wa kiuchumi.
Akizungumzia historia ya visiwa hivyo, Othman alieleza kuwa Zanzibar imepitia vipindi mbalimbali vya kihistoria ambavyo vinapaswa kutumika kama funzo la kujenga mustakabali bora badala ya kurudia makosa ya zamani.
Alisema kuwa wakati umefika kwa nchi hiyo kuandika hadithi mpya inayotokana na misingi ya maendeleo, mshikamano, na amani ya kweli, huku akiwakumbusha wajumbe wa kamati hiyo kuwa ndio waandishi wakuu wa misingi hiyo mipya itakayojenga heshima na utukufu wa Zanzibar.
Aidha, aliwataka viongozi na wadau wote kuweka kando itikadi za kisiasa na mirengo yao na kuutazama mchakato huo kama jukumu kubwa la kizalendo linalopaswa kutekelezwa kwa heshima ili kuliweka taifa mbele.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya kazi hiyo yataacha alama ya kudumu katika historia ya Wazanzibari, Watanzania, na dunia kwa ujumla.
Othman aliwapongeza marais wastaafu wa Zanzibar kwa hekima na busara zao zilizowezesha kufikia hatua hiyo ya maridhiano, huku akimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa baraka na usimamizi wake thabiti katika safari hiyo ya maridhiano, akiahidi kuwa chama cha ACT Wazalendo kitatoa ushirikiano kamili ili kuhakikisha malengo ya kamati hiyo yanafikiwa.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment