WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ametoa agizo kali la siku saba kwa Bodi ya Maji Bonde la Mto Rufiji kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa tuta katika Mto Lumemo, eneo ambalo maji yake yamekuwa tishio kwa usalama na mali za wananchi wa Kata ya Ipangalala, Wilaya ya Kilombero.
Masauni alitoa agizo hilo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro, iliyolenga kukagua kwa kina hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabili athari za mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.
Akizungumza kwa msisitizo, Waziri huyo alionya kuwa kuchelewa kukamilika kwa ujenzi huo kunaweza kuhatarisha maisha ya wananchi kutokana na taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazoashiria kuwepo kwa mvua za kishindo.
“Maisha ya binadamu ni muhimu sana kuliko fedha ambazo tutatumia kujenga eneo hili. Hivyo, natoa wiki moja wahusika wawe wamekamilisha ujenzi kwa kuwa muda uliopo si rafiki kutokana na utabiri uliotolewa kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha,” alisema Mhe. Masauni.
Sambamba na maagizo hayo, Waziri Masauni aliwakumbusha wananchi kuchukua jukumu la kulinda mazingira kwa kupanda miti na kuepuka utupaji holela wa taka, akibainisha kuwa tabia hiyo inachangia kuziba kwa mifereji na kusababisha maji kuhama mkondo na kuleta madhara makubwa kwenye miundombinu.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuwalinda wananchi na kutoa elimu endelevu ya kukabiliana na majanga ya mafuriko.
Kwa upande wake, Afisa wa Maji Bonde la Kilombero, Abisai Chilunda, alieleza kuwa tuta linalojengwa lina urefu wa takribani kilomita 11, na kwamba timu yake imejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa haraka katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwa kuweka mawe na kujaza udongo kwenye sehemu zilizopasuka. Aliongeza kuwa bonde lao limekuwa likishirikiana bega kwa bega na wananchi kudhibiti maeneo hatarishi kupitia ujenzi wa mifereji na matuta ya kupitishia maji salama.
Naye Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Elibariki Bajuta, aliwasihi wananchi wanaoishi mabondeni kuhamia maeneo salama mapema, huku akiwataka kuacha ukataji miti ovyo na matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kuziba mitaro ya maji.
Katika ziara hiyo, Mhe. Masauni na ujumbe wake walikagua maeneo mbalimbali yenye changamoto za kimazingira na miundombinu nchini, ikiwemo ujenzi wa tuta la Reli ya SGR kuanzia Mkundi hadi Lukobe, Mto Diwale katika Kata ya Kichangani (Turiani), eneo la Dumila katika Mto Kikundi, Mto Mkondoa–Kidete katika Kata ya Kasiki, na Mto Lumemo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
PROFESSOR MGOKO EPISODE 03
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment