Na.Mwandishi Wetu
Tume ya Ushindani ya Somali imefanya ziara ya siku moja nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza uzoefu na mbinu zinazotumiwa na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) katika kusimamia ushindani wa kibiashara, kudhibiti bidhaa bandia na kulinda maslahi ya walaji.
Ziara hiyo imefanywa na Mkurugenzi wa Masuala ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na Kamishna wa Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki (EACA), Bw. Ahmed Warsame pamoja na Mkurugenzi wa Biashara na Upatikanaji wa Masoko wa Wizara ya Biashara na Viwanda ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Bw. Abdihalim Osman.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo umekutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, pamoja na uongozi wa Tume, ambapo walipata fursa ya kujifunza namna FCC inavyotekeleza majukumu yake ya kukuza na kulinda ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, uongozi wa ujumbe wa Somalia umepongeza utendaji wa FCC, ukieleza kuwa uzoefu wa Tanzania katika kusimamia ushindani na kulinda mlaji ni muhimu kwa Somalia katika kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa soko na kukuza mazingira bora ya biashara.
Ujumbe huo umeeleza kuwa kujifunza kutoka FCC kutasaidia kuongeza uelewa na uwezo wa taasisi za Somalia katika kukabiliana na changamoto zinazohusu ushindani usio wa haki, bidhaa bandia na vitendo vinavyoweza kuwadhuru walaji.
Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema kuwa Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na taasisi za Somalia na nchi nyingine katika kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za usimamizi wa ushindani na ulinzi wa walaji.
Ziara hiyo ya siku moja imekuwa fursa muhimu kwa Somalia kujifunza uzoefu wa Tanzania katika eneo la ushindani wa kibiashara, udhibiti wa bidhaa bandia na ulinzi wa mlaji, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi na kuchangia katika ujenzi wa masoko yenye ushindani wa haki na biashara endelevu.
Post a Comment