" LAAC YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO JIJI LA DODOMA

LAAC YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO JIJI LA DODOMA

Na. Jesca Kipingu, DodomaKamati ya Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa (LAAC) imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, huku ikipongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia ubora, thamani ya fedha na mahitaji ya wananchi.Pongezi hizo zimetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Abdallah Chikota, wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ikiwemo ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.6 inayoelekea Hospitali ya Jiji la Dodoma katika eneo la Nala pamoja na ujenzi wa jengo jumuishi katika Kituo cha Afya Makole, ambalo linajengwa kwa mfumo wa ghorofa.Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Chikota aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa namna inavyotekeleza miradi hiyo, akieleza kuwa kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha pamoja na ubora wa kazi zinazofanyika.“Tunawapongeza kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo ambao umezingatia thamani ya fedha iliyotumika. Kwa upande wa barabara, mmejenga kwa kiwango kizuri na cha ubora, huku katika Kituo cha Afya Makole mmeonesha ubunifu mkubwa. Kutokana na ufinyu wa eneo, badala ya kujenga majengo ya kawaida ya chini, mmejenga jengo la ghorofa ambalo linaongeza uwezo wa kituo kutoa huduma na hatimaye kukifanya kiwe na hadhi ya hospitali,” alisema Chikota.Aidha, Chikota alieleza kuwa utekelezaji wa miradi yenye ubora na inayozingatia thamani ya fedha una mchango mkubwa katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma bora. Alisisitiza umuhimu wa Halmashauri kuendelea kusimamia miradi kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na inaleta matokeo yaliyokusudiwa.Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Vincent Odero, alisema ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kuelekea Hospitali ya Jiji la Dodoma – Nala umegharimu Shilingi bilioni 2.874. Alisema mradi huo unalenga kurahisisha usafiri na kuwawezesha wananchi kufika hospitalini kwa urahisi, pamoja na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya katika eneo hilo.Huku  ujenzi wa jengo jumuishi la kutolea huduma katika Kituo cha Afya Makole, Odero alisema mradi huo utakapokamilika utagharimu takribani Shilingi bilioni 6.9, ambazo zinatokana na fedha kutoka Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.Ziara hiyo ya Kamati ya Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa (LAAC) inalenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri, kujiridhisha kuhusu matumizi sahihi ya fedha za umma, ubora wa miradi na uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na viwango vinavyotakiwa katika utekelezaji wa miradi.

 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post