" MBUNGE LUPEMBE AENDELEA NA ZIARA NSIMBO, ATEMBELEA VIJIWE VYA KAHAWA KATAMBIKE NA KUNYWA KAHAWA NA WANANCHI

MBUNGE LUPEMBE AENDELEA NA ZIARA NSIMBO, ATEMBELEA VIJIWE VYA KAHAWA KATAMBIKE NA KUNYWA KAHAWA NA WANANCHI

Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Mkoa wa Katavi, Anna Richard Lupembe, Septemba 29, 2026 ameendelea na ziara yake ya kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara na kutembelea maeneo mbalimbali katika jimbo hilo, ikiwemo Kijiji cha Katambike, Kitongoji cha Kasilanya, Kichangani na Ugalla Senta.

Katika ziara hiyo, Lupembe amepata fursa ya kuwasalimia wananchi wa Kijiji cha Katambike, Kata ya Ugalla, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa karibu na wananchi na kusikiliza maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu katika maeneo yao.

Mbunge huyo pia ametembelea kijiwe cha kahawa kilichopo Katambike, ambapo alikutana na wazee na wananchi waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo kwa ajili ya kunywa kahawa, kubadilishana mawazo na kujadili masuala mbalimbali ya kijamii.

Lupembe alishiriki pamoja na wazee hao kunywa kahawa, akieleza kuwa vijiwe vya kahawa ni sehemu muhimu ya jamii kwa kuwa vinawawezesha wananchi kukutana, kuzungumza na kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo na changamoto zinazowakabili.

Aidha, Mbunge huyo amesema atafuatilia suala la kuboresha miundombinu ya vijiwe hivyo ili viwe katika mazingira bora na rafiki kwa wananchi wanaovitumia.

Katika ziara hiyo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Jimotoli Jilala Maduka, alimwakilisha Katibu wa CCM Wilaya ya Mpanda, Musa Ramadhan Mwevi, na kushiriki katika shughuli mbalimbali za ziara hiyo pamoja na Mbunge Lupembe.

Ziara hiyo imeendelea kuwa sehemu ya juhudi za Mbunge Lupembe za kuwasikiliza wananchi, kuwafahamu kwa karibu na kufuatilia masuala mbalimbali yanayohusu ustawi na maendeleo ya Jimbo la Nsimbo.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post