"
MR. BLACK AREJESHA TUMAINI KWA SHULE ZA MSINGI KITANGIRI NA BUGAYAMBELELE SHINYANGA
Mkurugenzi wa The BSL Investments Company Ltd na BSL Schools, Peter Frank Lugumi maarufu kama Mr. Black, ameendelea kuonesha dhamira yake ya kuwa mdau wa maendeleo katika sekta ya elimu kwa kutoa msaada kwa Shule za Msingi Kitangiri na Bugayambelele zilizopo Manispaa ya Shinyanga.Mr. Black ametoa msaada huo leo, Septemba 23, 2026, akiwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya shule hizo mbili, ambapo amegusa maeneo mbalimbali yenye mahitaji kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.Katika Shule ya Msingi Kitangiri, Mr. Black amekabidhi kompyuta mpakato (Laptop) kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya Mkuu wa Shule. Aidha, ameahidi kutoa vifaa vya michezo pamoja na viti kwa ajili ya walimu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuboresha mazingira ya kazi shuleni.Kwa upande wa Shule ya Msingi Bugayambelele, iliyopo katika Kata ya Kizumbi, amekabidhi fedha taslimu kwa ajili ya ununuzi wa Printer kwa matumizi ya shule. Pia ameahidi kutoa matofali 300 yatakayotumika katika ujenzi wa choo cha wanafunzi.Mbali na misaada hiyo, Mr. Black pia ameendesha harambee ya kuchangia maendeleo ya shule zote mbili, akihamasisha wazazi, walimu, viongozi na wadau mbalimbali kushirikiana katika kuboresha miundombinu na huduma za elimu.Katika hafla hizo, Mr. Black alitumia pia nafasi hiyo kutoa nasaha kwa wazazi, walimu na wanafunzi, akisisitiza umuhimu wa malezi bora, nidhamu, bidii katika masomo, pamoja na ushirikiano na mshikamano ndani ya jamii.«“Elimu ni msingi wa maendeleo ya mtoto, familia na jamii kwa ujumla. Tunapaswa kushirikiana kuhakikisha watoto wetu wanapata mazingira bora ya kujifunza na kukua,” alisema Mr. Black.»Aidha, Mr. Black ameahidi kuendelea kuwa mdau wa maendeleo wa shule hizo, akieleza kuwa msaada kwa elimu ni sehemu ya dhamira yake ya kushiriki katika kujenga jamii yenye fursa na maendeleo endelevu.Katika hatua nyingine yenye kugusa maisha ya moja kwa moja, Mr. Black amefadhili masomo ya wanafunzi wanne wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo watoto yatima, ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao bila kukatishwa na changamoto za kifedha.Hatua hiyo imeongeza nguvu katika juhudi za kuunga mkono elimu na ustawi wa watoto katika jamii ya Shinyanga, huku ikiendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, wazazi, jamii na wadau binafsi katika kuleta maendeleo ya elimu.
THE BSL INVESTMENTS COMPANY LTD & BSL SCHOOLS — KUWEKEZA KATIKA ELIMU, KUJENGA JAMII, KUCHOCHEA MAENDELEO.






























Post a Comment