
Na.Sophia Kingimali, Dar es Salaam.
JESHI la Polisi Nchini limesema mfumo wa kukata pointi kwenye leseni za madereva bado haujaanza kutekelezwa, licha ya madai yaliyoibuka miongoni mwa baadhi ya madereva kuwa hatua hiyo imeanza na kuchangia mvutano uliosababisha baadhi yao kusitisha huduma za usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 29/2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi anayeshughulikia Operesheni na Mafunzo, CP Awadh Juma Haji, amesema madai kwamba madereva wameanza kupoteza pointi kwenye leseni zao hayana msingi kwa sababu utekelezaji wa mfumo huo bado haujaanza.
Amesema kwa sasa kinachofanyika ni uelimishaji wa madereva na wananchi kuhusu mfumo huo ambao umewekwa kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa taarifa rasmi itatolewa wakati utekelezaji wake utakapoanza.
“Mpaka sasa hakuna dereva ambaye leseni yake imeondolewa kwa kukatwa pointi. Jambo hilo bado halijaanza kutekelezwa,” amesema CP Haji.
Kamishna Haji amesema lengo la mfumo huo ni kuimarisha usalama barabarani kwa kudhibiti madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani na ambao uendeshaji wao unaweza kuhatarisha maisha ya watu na mali.
Amesema madereva wanaofuata sheria hawana sababu ya kuwa na hofu kuhusu mfumo huo, akisisitiza kuwa utakapofika wakati wa utekelezaji, taratibu za kisheria zitatumika na madereva watapewa taarifa rasmi.
Aidha, amesema dereva ambaye atahisi ameonewa wakati wa utekelezaji wa mfumo huo atakuwa na haki ya kuwasilisha malalamiko yake kwa mamlaka husika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Wakati akitoa ufafanuzi huo, Kamishna Haji pia ameonya watu wanaotumia mvutano huo kuzuia mabasi, malori na magari mengine kusafiri, akisema Jeshi la Polisi litachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria.
Amesema makamanda wa polisi wa mikoa yote wameelekezwa kufuatilia hali hiyo na kuhakikisha usalama wa madereva, abiria na magari unaendelea kuwepo, huku akiwataka madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuendelea na shughuli zao bila hofu.
PROFESSOR MGOKO EPISODE 03
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment