Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amesema kuwa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kunalenga kuongeza kasi ya maendeleo, huku Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, akisisitiza kuwa hatua hiyo si ya kugawana vyeo bali ni mwanzo wa safari ya pamoja ya kujenga Zanzibar inayostahili kupitia dhamira ya dhati na ushiriki wa kila mwananchi.
Kauli hizo zilitolewa katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, tukio lililoshuhudiwa na viongozi mbalimbali na wadau wa siasa.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa kwake, Othman alieleza kuwa serikali hiyo haikukusudiwa kuwa chombo cha kugawana vyeo kwa ajili ya kambi za kisiasa, bali ilianzishwa ili kusimamia, kuratibu, na kuongoza juhudi za Wazanzibari kufikia maridhiano na umoja wa kitaifa, pamoja na kutoa ufahamu sahihi kwa wale wote wenye mitazamo potofu kuhusu mfumo huo. Aliongeza kuwa kukamilishwa kwa uundaji wa serikali hiyo na uteuzi wa mawaziri hakuhitimishi safari ya watu wa Zanzibar, bali kunaanzisha safari muhimu inayohitaji ukweli, uelewa, na ushiriki thabiti wa kila mwananchi bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
Othman alibainisha kuwa mchakato huo wa maridhiano haupaswi kuchukuliwa kama wa faida ya vyama vya siasa pekee, bali unapaswa kuangalia mageuzi ya kiulimwengu, mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia, pamoja na jinsi Zanzibar inavyoweza kunufaika na mabadiliko hayo.
Alitolea mfano jinsi nchi ambazo hapo awali zilikuwa maskini barani Asia, Amerika ya Kusini, na Afrika zinavyopiga hatua kubwa za maendeleo, akawakumbusha viongozi na watendaji serikalini kufanya uteuzi na chaguzi za viongozi wanaowafaa, wenye uchungu na nchi, na wanaoweka mbele maslahi ya taifa ili kuendesha mambo kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kuwa uamuzi wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa unatokana na maridhiano yaliyofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, yaliyowezesha kusainiwa kwa Tamko la Pamoja la Maridhiano, hatua inayotimiza matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ya toleo la 2010. Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa serikali hiyo mpya inatambua uwepo wa tofauti za kisiasa lakini inaweka mbele maslahi mapana ya nchi, ikiwataka wananchi na viongozi wote kuelekeza nguvu zao kwenye kazi ya kujenga nchi na kuleta maendeleo endelevu.
Akizungumzia utamaduni wa Zanzibar wa kutatua changamoto kupitia mazungumzo, Dk. Mwinyi alikumbusha mafanikio ya maridhiano ya mwaka 2010, akisisitiza kuwa maridhiano si mwisho wa safari bali ni mwanzo wa kazi kubwa ya kuvuka daraja la kisiasa na kusonga mbele pamoja.
Alitoa maagizo madhubuti ya kuongeza kasi ya kukuza uchumi, kuzalisha ajira na fursa zaidi kwa vijana, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuimarisha sekta ya utalii, kuendeleza uchumi wa buluu, kuvutia wawekezaji, na kuboresha huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, na nishati.
Aidha, Dk. Mwinyi alitoa shukrani za dhati kwa vyama vyote vya siasa visiwani humo kwa kuunga mkono maridhiano na kuonyesha utayari wa kushirikiana, akisema hatua hiyo inadhihirisha ukomavu mkubwa wa kisiasa na uwezo wa Wazanzibari wa kutatua migogoro yao wenyewe.
Aliwashukuru pia wajumbe wa kamati iliyoratibu mazungumzo hayo pamoja na viongozi wastaafu, wakiwemo marais wastaafu Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein, pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, kwa mchango wao mkubwa wa hekima, uzoefu, na busara katika kufanikisha mchakato huo wa kihistoria.
PROFESSOR MGOKO EPISODE 2
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment