" Tanzania Yaeleza Mikakati ya Kuunganisha Rasilimali za Gesi na Masoko ya Kimataifa

Tanzania Yaeleza Mikakati ya Kuunganisha Rasilimali za Gesi na Masoko ya Kimataifa




Serikali imeeleza kuwa Tanzania imeanza hatua madhubuti za kuunganisha rasilimali zake za gesi na masoko ya dunia huku ikisisitiza kuwa matumizi ya gesi katika soko la ndani na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuuza nje havipaswi kuonekana kama mikakati inayokinzana, bali ni sehemu jumuishi ya kukuza uchumi wa taifa.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alipokuwa akishiriki mjadala wa kimataifa katika Mkutano wa Gastech 2026 unaofanyika mjini Bangkok, Thailand, ambapo alieleza kuwa matumizi ya gesi kwa sasa nchini yanajumuisha asilimia 69 katika uzalishaji wa umeme, asilimia 27 viwandani, asilimia tatu katika usafirishaji, na asilimia moja katika taasisi na kaya, jambo linaloonyesha gesi inavyotumika kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda na usalama wa nishati.

Naibu Waziri alifafanua kuwa masoko ya ndani na ya kikanda yanatoa manufaa ya haraka ya kiuchumi na kujenga uwezo wa ndani, wakati miradi mikubwa ya kuuza nje inafungua milango ya uwekezaji mkubwa na teknolojia ya kimataifa, akisisitiza kuwa historia ya nchi kuanzia ugunduzi wa Songo Songo miaka ya 1970 na kuanza uzalishaji mwaka 2004 inaonyesha rasilimali pekee haitoshi bila miundombinu, sera rafiki, na ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Tanzania yenye zaidi ya trilioni 57 za futi za ujazo za gesi asilia iliyogunduliwa zaidi katika maeneo ya bahari kuu, pamoja na maeneo ya Songo Songo na Mnazi Bay, inatumia vyanzo hivyo kufua umeme na kuongeza matumizi ya gesi asilia iliyosindikwa (CNG) kwenye sekta ya usafirishaji na kaya.

Alihitimisha kwa kueleza kuwa nchi zitakazofanya vizuri kwenye sekta ya gesi si lazima ziwe zenye rasilimali nyingi pekee, bali zile zenye mikakati bora ya uwekezaji, miundombinu thabiti, na ushirikishwaji mpana wa wananchi, ambapo Tanzania inasimama vyema kutokana na nafasi yake ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Post a Comment

Previous Post Next Post