" WAZAZI WATAKIWA KUWA NA MOYO WA KUWEKEZA KATIKA ELIMU

WAZAZI WATAKIWA KUWA NA MOYO WA KUWEKEZA KATIKA ELIMU

                         


                       NA FAUZIA MUSSA

    WAZAZI na walezi wametakiwa kuwa na moyo wa kujitoa na kuwekeza katika elimu ya vijana wao ili kuwawezesha kupata mazingira bora ya kujisomea na kufanya vizuri katika mitihani yao.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Magharibi, Tauhida Cassian Gallos Nyimbo, wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya lazima kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaoshiriki kambi za masomo katika Skuli ya Sekondari Mwenge na Mfenesini, Mkoa wa mjini Magharibi.

Vifaa vilovyokabidhiwa ni pamoja pad, Mchele, mafuta, sukari, maharage na sabuni ya kufulia.

Tauhida alisema baadhi ya wanafunzi hushindwa kushiriki katika kambi hizo kutokana na kutomudu gharama za mahitaji muhimu, jambo alilosema linahitaji wazazi na walezi kuwa na mwamko wa kuwekeza katika elimu ya watoto wao.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona mwanafunzi anakosa fursa ya kushiriki katika kambi ya masomo kwa sababu ya kukosekana kwa mahitaji, huku akisisitiza kuwa wazazi hawapaswi kuona gharama za elimu kama mzigo bali uwekezaji wa maisha ya watoto wao.

Aidha aliwashauri walimu na walezi kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mahitaji Katika kambi hizo, badala ya kutegemea fedha pekee, huku akiwataka kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi ambao wameshindwa kushiriki kwa sababu ya changamoto za gharama.

“Tatizo si pesa, tatizo ni moyo wa kujitoa, utayari na mashirikiano. Mmoja akileta kuni mwengine analeta nazi, mihogo, ndizi na mwengine anatoa fedha Kwa pamoja vinasaidia kuwafanya vijana wetu waishi Kwenye kambi hizi” alisema Tauhida 

Pamoja na hayo, aliwasihi wanafunzi waliopata nafasi ya kushiriki kambi hizo kuwa na moyo wa kuwasaidia wenzao ambao hawakuweza kushiriki, akieleza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kutoa sadaka na kutarajia malipo kutoka kwa Allah.

Vile vile Tauhida aliwataka wanafunzi kuwa na malengo yatakayowasukuma kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao, huku akiwashauri kuwatii walimu,wazazi na walezi wao kwa kuwa elimu wanayoipata kwao ni maandalizi ya maisha yao ya baadaye.

“Mnapaswa kuthamini juhudi zinazofanywa na wazazi, walezi na walimu wenu, mafunzo wanayowapatia ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na changamoto za maisha Yenu siku za baadae.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Jimbo la Mfenesini, Bahati Hussein Abdalla, Alisema wataendelea kushirikiana na viongozi, walimu na wazazi kuhakikisha wanafunzi wote wanaotarajia kufanya mtihani wanapata fursa ya kushiriki katika kambi hizo kwa lengo la kuimarisha ufaulu.

Aidha aliwataka wanafunzi hao kutokata tamaa na kusoma kwa bidii ili kuhakikisha wanaondoa kiwango cha ufaulu wa daraja sifuri katika skuli hizo na jimbo la mfenesini Kwa ujumla.

Kwa kuwa kambi hizo zinawahusisha wanafunzi wa jinsia zote, Bahati aliwasisitiza vijana kuepuka vitendo visivyohusiana na masomo, ikiwemo kuingia katika mahusiano ya kimapenzi, akieleza kuwa vinaweza kuwafanya kupoteza mwelekeo na kuathiri masomo yao.

Walimu wa skuli hizo walishukuru wajumbe kwa ziara hiyo walioitaja kuwa haikua ya kuleta msaada pekee Katika kambi hizo bali sehemu ya hamasa na kuamsha ari Kwa wanafunzi wao kusoma Kwa malengo.

Walisema kambi hizo zimekuwa zikisaidia kuongeza umakini wa wanafunzi katika masomo na kuongeza kiwango cha ufaulu licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbalimbali.

Akielezea baadhi ya changamoto hizo Msaidizi Mwalimu Mkuu skuli ya Sekondari Mwenge, Sheha Ali Khamis, alisema uzoefu unaonesha kuwa kambi nyingi za wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya kidato cha nne zinakosa uwezo WA kukidhi mahitaji muhimu, kama chakula hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kushiriki.

Akitolea mfano wa skuli ya mwenge alisema kati ya wanafunzi 53 wanaotarajiwa kufanya mitihani wa kidato cha nne katika skuli hiyo wanafunzi 25 pekee ndio walioweza kuchangia na kushiriki katika kambi ya masomo skulini hapo.

Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Jimbo la Mfenesini walimpongeza Tauhida kwa msaada huo unalenga kuunga mkono jitihada za walimu, wazazi na walezi Katika kukidhi mahitaji muhimu ya wanafunzi ili kuwapa nafasi ya kujikita katika masomo bila kulazimika kujishughulisha na kutafuta mahitaji hayo wakati wa kambi.

Wajumbe hao walisisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali kushirikiana kuhakikisha wanafunzi wote wanapata fursa ya kunufaika na kambi hizo na kujiandaa vyema kwa mitihani ya Kidato cha Nne inayotarajiwa kuanza Novemba 9, 2026.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652


Post a Comment

Previous Post Next Post