" BALOZI YAKUBU AKUTANA NA MWENYEKITI WA BODI YA UTENDAJI YA UNESCO

BALOZI YAKUBU AKUTANA NA MWENYEKITI WA BODI YA UTENDAJI YA UNESCO

 Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Saidi Yakubu, amekutana kwa mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya UNESCO, Dkt. Nasser Hamad Al Hinzab, jijini Paris, Ufaransa.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walibadilishana mawazo kuhusu namna ya kuendeleza michezo, utamaduni, elimu na sayansi kupitia mamlaka na programu za UNESCO. Walijadili pia umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi wanachama katika kuhakikisha shughuli za Shirika hilo zinakidhi mahitaji na vipaumbele vya maendeleo vya wananchi.

Bodi ya Utendaji ni chombo muhimu katika uongozi wa UNESCO, chenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano Mkuu, kutathmini programu na makadirio ya bajeti ya Shirika, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake. Mwenyekiti wa Bodi ana nafasi muhimu ya kuongoza mijadala, kuratibu kazi za Bodi na kuwezesha nchi wanachama kufikia maelewano kuhusu masuala yanayohusu mwelekeo na utendaji wa UNESCO.

Mazungumzo hayo yalikuwa fursa kwa Balozi Yakubu kuelewa umuhimu wa kutumia majukwaa ya UNESCO kuendeleza vipaumbele vya Tanzania katika elimu, sayansi, utamaduni na michezo, pamoja na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika shughuli za Shirika hilo.

Dkt. Nasser, ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Qatar katika UNESCO, alimweleza Balozi Yakubu kuwa maandalizi ya Mkutano wa Bodi ya Utendaji unaotarajiwa kuanza Jumatatu yamekamilika. Mkutano huo utatoa nafasi kwa nchi wanachama kujadili masuala muhimu yanayohusu programu, usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya UNESCO.