" BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI,REA KUTEKELEZA MIRADI YA NISHATI

BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI,REA KUTEKELEZA MIRADI YA NISHATI


📍Mwanza

Benki ya Dunia yaipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini pamoja na utekelezaji wa miradi ya kuwawezesha sekta binafsi kuzalisha umeme nchini.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mkoani Mwanza na Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia ambaye pia ni Mtaalam wa Nishati, Dkt. Rhonda Jordan wakati wa ziara ya ujumbe huo kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo na kusimamiwa na REA.

“Tumekuwa na vikao na REA kupata taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo inafadhiliwa na Benki ya Dunia. Tumekuja kutembelea na kuona miradi hiyo na maendeleo yake. Moja ya mradi tuliotembelea leo ni mradi wa waendelezaji wadogo waliowezeshwa na REA ambao wanazalisha umeme kwa kutumia mfumo wa jua na kuingiza katika gridi ya Taifa.

Wazalishaji kama hawa wana mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo ya jamii. Tunawapongeza REA kwa usimamizi wa miradi hii na tunaahidi kuendelea kushirikiana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na REA kuendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kunakuwa na nishati ya uhakika kwa maendeleo endelevu,” amesema Dkt. Rhonda.

Awali akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Bugando Natural Energy Limited na kusimamiwa na REA unazalisha jumla ya Megawati 5 ambazo zinaingizwa kwenye gridi ya Taifa ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme.

Mhandisi Mwijage amesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini imekuwa ikipata fedha kutoka kwa Wabia mbalimbali wa Maendeleo kama Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyolenga kuendelea kuboresha maisha ya wananchi maeneo mbalimbali.

“Sisi kama REA tumefarijika sana kufika katika mradi huu pamoja na Wabia wetu wa Maendeleo ambao walitoa fedha za kuwezesha kutekelezwa kwa mradi huu. Mradi huu ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali kuhakikisha kuna kuwa na nishati ya umeme ya uhakika na endelevu kuwezesha malengo mbalimbali yaliyowekwa na Serikali yanaweza kufikiwa,” amesema Mhandisi Mwijage.

Mhandisi Mwijage amewashukuru Wabia wa Maendeleo wakiwamo Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini huku akiahidi kuwa wataendelea kusimamia fedha zinazotolewa kwa usahihi ili kuweza kuleta matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

       

Post a Comment

Previous Post Next Post