" RC HAMDUNI:NISHATI NI KICHOCHEO KIKUBWA CHA MAENDELEO

RC HAMDUNI:NISHATI NI KICHOCHEO KIKUBWA CHA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP. Salum Hamduni amesema kuwa nishati ni kichochea kikubwa cha maendeleo na uboreshaji wa huduma za kijamii.

Mkuu wa Mkoa Hamduni amesema hayo leo wakati wa kikao na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia ulipofika Ofisini kwake kabla ya kuanza ziara ya kukagua maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo inayotekelezwa na REA katika Mkoa huo.

“Sekta ya nishati ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa sekta nyingine. Hatuwezi kuzungumza maendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika. Kwenye hili sisi kama Mkoa tunaendelea kuipongeza Wizara ya Nishati na hususani REA kwa kazi kubwa mnayoendelea kuifanya.

Lakini pia tumshkuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha utekelezwaji wa miradi hii ya upelekekaji wa umeme vijijini. Tunaendelea pia kuwashkuru sana Wabia wa Maendeleo kama Benki ya Dunia kwa michango yao katika utekelezwaji wa miradi ya nishati,” amesema Mhe. Hamduni.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe huo ambaye pia ni Mtaalam wa Nishati kutoka Benki ya Dunia, Rhonda Jordan ameahidi kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha maisha wananchi kupitia upatikanaji wa nishati kwa maendeleo yao.

Awali akitoa taarifa kuhusu utekelezwaji wa miradi inayotekelezwa na REA katika Mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage amesema kuwa katika Mkoa wa Mwanza Wakala umefanikiwa kufikisha umeme katika Vijiji vyote na kwa sasa REA inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji.

Kwa mujibu wa Mhadisi Mwijage, kati ya vitongoji 3448 vilivyopo mkoani Mwanza, vitongoji 1597 tayari vimefikishiwa umeme huku vitongoji 619 Wakandarasi wako katika maeneo hayo wakiendelea na kazi.

Mhandisi Mwijage ameongeza pia, kwa Mkoa wa Mwanza REA kwa kushirikiana na Wabia wa Maendeleo umeanza utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme kwa wananchi waishio visiwani.

“Mkoa wa Mwanza una wananchi wengi wanaoishai visiwani. Serikali kupitia REA imeanza utekelezaji wa mradi wa kuwafungia mifumo ya umeme jua kwa bei ya ruzukua ambapo serikali inatoa ruzuku ya kuanzia asilimia 45 mpaka asimilia 75.” Amesema Mkurugenzi Mwijage.

      

Post a Comment

Previous Post Next Post